NA KHAMISUU ABDALLAH

ALIYEDAIWA kutapeli mamilioni ya pesa Mshitakiwa Khamis Shkeli Masoud (50) mkaazi wa Chuini wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, amefikishwa katika mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo alifikishwa Mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mummin Ali Juma, na kusomewa mashitaka yanayomkabili na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Said Ali.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na makosa mawili ya wizi baada ya kuaminiwa kinyume na kifungu cha 274 (7) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa siku na tarehe isiyofahamika mwaka 2013 saa 5:00 asubuhi huko Nyerere mshitakiwa huyo aliaminiwa na kukabidhiwa fedha taslimu shilingi 15,000,000 mali ya Kiumbwa Makame Mbaraka kwa lengo la kumnunulia gari aina ya basi (Rosa) kitendo ambacho hakukifanya jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mwendesha Mashitaka Wakili Soud, alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa jengine la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambapo siku isiyofahamika mwaka huo huo majira ya saa 12:00 jioni huko Nyerere aliaminiwa na kukabidhiwa shilingi 12,000,000 na mlalamikaji huyo kwa lengo la kutoa gari hiyo Bandarini Malindi Unguja kitendo ambacho hakujikifanya.

Mshitakiwa huyo aliposomewa mashitaka hayo aliyakataa na kuiomba mahakama impatie dhamana kwa madai kuwa anategemewa katika familia.

Mwendesha Mashitaka Said aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Akizungumzia suala la kupatiwa dhamana kwa mshitakiwa huyo DPP Said alisema upande wa mashitaka hauna pingamizi ikiwa mshitakiwa huyo atapewa masharti ambayo yatamfanya kufika mahakamani kila tarehe ya kesi yake.

Hakimu Mummin alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 taslimu na kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi mmoja awe ni mfanyakazi wa serikali na kuwasilisha vitambulisho vyao vya mzanzibari mkaazi.

Mahakama iliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 8 mwaka huu na kuamuaru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.