PARIS,UFARANSA

WANAJESHI  wawili wa Ufaransa wameuawa huku mwengine mmoja akijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi huko kaskazini mwa Mali.

Hayo yalitangazwa na Ofisi ya Rais wa Ufaransa ambayo ilisema, askari hao waliuawa baada ya gari lao la doria kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini katika eneo la Tessalit, kaskazini mwa Mali.

Wanajeshi hao wa Ufaransa waliouawa walikuwa sehemu ya vikosi vinavyoendesha Operesheni ya Barkhane yenye lengo la kutokomeza makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwapongeza wanajeshi wa Ufaransa walioko katika eneo hilo kwa kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya vita dhidi ya ugaidi, huku akitoa wito wa kuundwa haraka iwezekanavyo Serikali ya mpito ya kiraia nchini Mali.

Ifahamike kuwa, maeneo ya kaskazini na katikati mwa Mali yalikumbwa na machafuko kutokana na kuweko magenge ya kigaidi yenye uhusiano na mitandao ya kigaidi ya al Qaida na Daesh (ISIS) ambayo mara kwa mara yanafanya mashambulio na mauaji ya kutisha dhidi ya wananchi na maofisa wa Serikali.

Hivi sasa mkoloni mkongwe wa Ulaya yaani Ufaransa ana wanajeshi 5,100 katika eneo hilo la Sahel Afrika lakini machafuko yanaendelea, yamekuwa makubwa zaidi, suala ambalo linawafanya wachambuzi wa mambo waamini kuwa, wanajeshi wa Ufaransa hawako katika eneo hilo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wala kwa ajili ya kupambana na magenge ya kigaidi, bali yako huko kwa ajili tu ya kulinda maslahi ya kikoloni ya Ufaransa.