NA KHAMISUU ABDALLAH
BAADA ya mshitakiwa John Samuel Manga (45) mkaazi wa Fuoni Migombani Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kukimbia mahakamani hatimae akamatwa na kupelekwa rumande.
Mshitakiwa huyo ambae anakabiliwa na shitaka la kujifanya Ofisa Usalama anaetoa ajira katika tasisi ya Usalama wa Taifa alimbia mahakamani hapo Agosti 24 mwaka huu kesi yake ilipofikishwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Hakimu Mohammed Subeit, anaesikiliza kesi hiyo alitoa oda ya kukamatwa kwa mshitakiwa huyo na kufikishwa mahakamani, ili kuendelea kusikiliza kesi yake inayomkabili.
Septemba 7, mwaka huu, mshitakiwa huyo alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Mwanakwerekwe na Septemba 9, alifikishwa mahakamani kuendelea na kesi yake na mahakama kuamuru kupelekwa rumande hadi Septemba 23 mwaka huu.
Awali mshitakiwa huyo alipewa dhamana ya kujijidhamini mwenyewe kwa maandishi kwa shilingi 5,000,000 na kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na barua za Sheha wa Shehia wanazoishi masharti ambayo aliyatimiza.