NA KHAMISUU ABDALLAH

FAINI ya shilingi 100,000 imemtoka mshitakiwa Ali Maftaha Uled mkaazi wa Mwera baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuendesha Handa akiwa hana leseni ya udereva.

Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 57, alitozwa faini hiyo na mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Naseem Faki Mfaume, baada ya kukubali kosa lake hilo na kutiwa hatiani kwa mujibu wa sheria.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Nassem alimtaka mshitakiwa huyo kulipa faini hiyo na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi miwili.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda jela kwa muda huo.

Kabla ya hukumu hiyo mshitakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kuendesha chombo cha moto ikiwa hakina leseni ya njia kinyume na kifungu cha 35 (1) (2) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Mwendesha Mashitaka wa Polisi Salum Ali aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo akiwa anaendesha honda yenye namba za usajili Z 721 KD akitokea Mwera Mtendeni kuelekea Mwera Magetini alipatikana akiwa anaendesha honda hiyo barabarani ikiwa haina leseni ya njia kitendo ambacho ni kosa kisheria.