NA KHAMISUU ABDALLAH

SULEIMAN Mohammed Suleiman (26) mkaazi wa Tomondo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa mjini Magharibi Unguja, amekamatwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani akikabiliwa na mashitaka matatu tofauti ya usalama barabarani.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume na kusomewa mashitaka yake na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Mwalim Gharib.

Kosa la kwanza ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana akiwa anaendesha vespa barabarani ikiwa hana leseni ya udereva ambapo kufanya hivyo ni kinyume na kifungu cha 81(1)(3) cha sheria namba7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa Suleiman alidaiwa kuwa Agosti 5 mwaka huu saa 4:30 asubuhi huko Mombasa kwenye mzunguko wa barabara akiwa dereva wa vespa yenye namba za usajili Z 377 BD akitokea Mombasa Sokoni kuelekea Mbuyumnene alipatikana akiendesha Vespa hiyo barabarani akiwa hana leseni ya udereva kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mwendesha Mashitaka Koplo Mwalim Gharib alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana akiendesha chombo cha moto akiwa hana leseni ya njia kinyume na kifungu 35 (1) (2) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Alidaiwa kuwa siku hiyo hiyo mshitakiwa huyo alipatikana akiendesha vespa hiyo barabarani akiwa hana leseni ya njia na chombo chake kukosa bima kitendo ambacho ni kosa kisheria

Shitaka la kuendesha vespa barabarani ikiwa haina bima, ni kosa kinyume na kifungu cha 3(1)(2) sura ya 136 sheria za bima.