LONDON, England
HATIMAYE nahodha na mshambuliaji wa Arsenal, Pierre Emerick Aubameyang amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake makuu Kaskazini mwa jijini London.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Gabon amesaini mkataba mpya, baada ya kukamilisha mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo, ambao ulionyesha kila sababu ya kutaka kuendelea kufanya kazi na nyota huyo, ambaye alisajiliwa mwaka 2018, akitokea Borussia Dortmund chini ya Arsene Wenger.

Aubameyang mwenye umri wa miaka 31 ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal hadi mwaka 2023, baada ya kusaini dili hilo ambalo litamfanya awe analipwa mshahara wa pauni 250,000 kwa wiki.

“Mwisho wa siku nimesaini moja ya saini kubwa, nina furaha kuwa ndani ya Arsenal. Hapa ni nyumbani na ni furaha kwangu”, alisema, Aubameyang.

“Siku ya leo (jana) ni kubwa kwangu na ninahitaji kuwa ‘nguli’ndani ya Arsenal na nitakapoondoka niache alama. Ni muda wangu wa kazi na nitapambana.”

Kabla ya kusaini mkataba mpya, Aubameyang alihusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu za ndani na nje ya England huku miamba ya Ligi Kuu ya Hispania, Real Madrid na Barcelona wakitajwa na vyombo vya habari.

Mshambuliaji huyo amekuwa na kiwango kikubwa huku akiwasaidia washika bunduki hao kutwaa mataji mawili likiwemo Kombe la FA.

Nyota huyo juzi alianza kufungua akaunti ya magoli msimu huu wakati Arsenal ikiilaza Fulham magoli 3-0 kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya England.(BBC Sports).