NA MADINA ISSA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema kuimarishwa kwa matamasha mbalimbali ya utamaduni ndani ya mkoa huo ikiwemo tamasha la mwaka kogwa, yameanza kuleta tija kwa wananchi wa vijiji vya mkoa huo kusaidia huduma muhimu za kijamii.

Aliyasema hayo, mara baada ya kukabidhi fedha taslim zilizotolewa na kamati ya mwaka kongwa kwa walimu wakuu wa skuli saba za vijiji vya Makunduchi,wenyeviti wa kamati za mashauriano ya vijiji hivyo pamoja na uongozi wa hospitali ya wilaya ya makunduchi.

Alisema imezoeleka kwamba matamasha mengi hufanyika kama ni sehemu ya utamaduni pekee, hali inayopelekea kutoleta tija za kimaendeleo kwa wazawa wa vijiji vinavyoanzisha matamasha,hivyo hatua hiyo itasaidia kurudisha imani kwa jamii juu ya ukuzaji wa matamasha hayo.

Aidha alisema Serikali kwa kushirikiana na kamati za matamasha hayo zimefikia hatua za kubadilisha taswira na kufanya yawe endelevu zaidi, ili kuyatengenezea vyanzo vya mapato vitakavyosaidia huduma mbalimbali za kimaendeleo katika vijiji hivyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya mwaka kogwa, Mwita Masemo alisema lengo la kutolewa fedha hizo ni kuona jamii inanufaika na makusanyo yaliyopatikana mwaka huu kupitia tamasha hilo ili ziweze kuisaidia jamii .

Nao baadhi ya waliopatiwa fedha hizo wameishukuru kamati hiyo kwa kuwapatia fedha hizo ambapo wameahidi kuzitumia kwa makusudio yaliyokusudiwa.

Tamasha la mwaka kogwa hufanyika kila mwaka ambapo huhudhuriwa na wageni kutoka mataifa mbalimbali.