Magufuli, Museveni wataka wananchi kutoa ushirikiano

Wananchi Mkoa wa Tanga wakaa tayari kuchangamkia fursa za ajira

NA MWANDISHI WETU, TANGA

HATIMAYE viongozi wa Tanzania na Uganda wamekubaliana kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka mji wa Hoima nchini Uganda hadi Changalieni mjini Tanga Tanzania.

Katika makubaliano hayo yaliotiwa saini na mawaziri wa nishati kutoka pande hizo mbili na marais wa mataifa hayo mawili John Pombe Magufuli wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda katika eneo la Chato, asilimia 60 ya faida ya mafuta hayo itaenda kwa Tanzania huku asilimia 40 ikienda kwa Uganda.

Akizungumza katika hafla hiyo, rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema kwamba cha muhimu ilikuwa kuanza mradi huo aliodai kucheleweshwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

“Niliamua kwamba kucheleweshwa kwa mradi huu kwasababu ya zile dola milioni 800 sio jambo la akili kwa sababu tunazugumzia kuzalisha mapipa bilioni 6.5 ikiwa ni asilimia 40 pekee ya mafuta yaliogunduliwa katika eneo la Albert, lakini huenda tukapata mafuta hata zaidi katika eneo hilo”, alisema.

Kiongozi huyo alisema kwamba uwekezaji wa bomba hilo la mafuta utagharimu dola bilioni 4 za Marekani.

“Niliamua kwamba wacha tuwache kuchelewesha tuanze mradi, tuliongea kwa simu mimi na mdogo wangu, nikamwambia achukue hata asilimia 70 au 80 lakini mdogo wangu akaona aibu akasema hapana, ni asilimia 60 itakwenda Tanzania, 40 nayo ikisalia na Uganda”, alisema.

Awali akizungumza, mara baada ya kutiliana saini Rais Magufuli, alisema kwamba mradi huo utaimarisha uchumi wa mataifa haya mawili na eneo lote la Afrika Mashariki na Kati.

Bomba la mafuta

Alisema kwamba mataifa yaliopo katika ushoroba wa kaskazini yatafaidika pakubwa na bomba hilo.

Aidha Rais Magufuli alisema kwamba takriban Watanzania kati ya 10,000 na hadi 15,000 watafaidika na ajira za kazi mradi huo utakapokamilika.

Aliongezea kwamba bomba hilo litakuwa na refu zaidi duniani linalotumia teknolojia ya kupasha moto mafuta likiwa na urefu wa kilomita 1,445.

“Litakuwa bomba refu zaidi duniani lenye teknolojia ya sasa ya kusafirisha mafuta yakiwa katika joto”, alisema raia Magufuli

Aidha taarifa hizo ziliongeza kuwa Kilomita 1,115 za bomba hilo zitakuwa upande wa Tanzania huku kilomita 330 zilizosalia zikiwa upande wa Tanzania.

Rais Magufuli aliongeza kwamba mradi huo utapitia mikoa minane ikiwemo wilaya 24. Mikoa hiyo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Magufuli alisema kwamba Watanzania 90,000 watakaoathiriwa mashamba yao watalipwa fidia ya bilioni 21 fedha za Tanzania.

Aliongezea kwamba Ujenzi wa vituo 14 vya bomba hilo vitawafidia watakaoathiriwa ambazo ni shilingi bilioni 9.9 za Tanzania.

Kwa kuwa mradi huu utaunufaisha pia Mkoa wa Tanga hivyo wanatarajia kupokea fursa kubwa ya kiuchumi ya mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga.

Mradi huo unaotarajiwa kutoa fursa kubwa ya kiuchumi pamoja na maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla unatarajiwa kujengwa katika eneo la Chongoleani lililopo nje Kidogo ya Jiji Tanga.

Wataalamu kutoka kampuni ya Total pamoja na washirika wao wapo Mkoani humo wataendelea na utafiti huo kwa kuanzia katika eneo la Chongoleani pamoja na njia ya ambayo itapitiwa na bomba hilo.

Hata hivyo Kwa upande wa Tanzania, Shirika la Maendeleo la Petroli TPDC ni sehemu ya washirika katika mradi huo ambapo mara baada ya mchakato wa ujenzi kukamilika kutauundwa kampuni ambayo itakuwa na dhamana ya kusimamia mradi huo.

Nae Mwanasheria Mwandamizi kutoka Shirika la Maendeleo la Petroli nchini TPDC, Kelvin Gadi, alisema kuwa hatua hiyo ya utafiti wa njia pamoja na eneo litakalojengwa miundombinu ya matangi na bandari ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo.

Alisema kuwa utekelezaji huo umeanza baada ya nchi zote mbili kutiliana saini ya makubaliano ya kisheria ya kufungua njia katika maeneo ambayo yatapita bomba hilo.

Aliongeza kuwa timu nyingine ya wataalamu wameanza kukagua na kufanya utafiti wa kimazingira katika eneo litakalo jengwa miundombinu ya kibandari katika eneo la Chongoleani.

“Kwa sasa wataalamu wanaendelea na upimaji wa udongo katika pwani ya bahari ya hindi eneo la Chongoleani na katika eneo lote litakalotumika kuweka miundombinu ya bomba hilo pamoja na kujua ukubwa wa eneo litakalotumika”, alisema Gadi.

Aliongeza kuwa eneo la awali lililopatikana kwa ajili ya kupitisha bomba lina upana wa kilomita mbili hivyo linatarajiwa kupunguzwa hadi kufikia mita mmoja ambalo ndilo linalohitajika.

Alisema kuwa mradi huo mpaka sasa upo katika hatua nzuri za kuanza utekelezaji wake hivyo wananchi wa Tanga wajiandae katika kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazo jitokeza. 

“Mradi huo unatarajia kunufaisha upande wa Tanzania kwa kiasi kikubwa kwani ukiangalia km zaidi ya 1443 zipo upande wa kwetu huku upande wa Uganda ni Km 296 pekee”, alisema Gadi.

Alifahamisha kuwa hivyo kuna uwezekano mkubwa watanzania wengi wakapata fursa ya ajira wakati wa ujenzi na katika kipindi cha usimamizi wa miundombinu yake”, alisema Mwanasheria huyo. 

Kwa upande wake Afisa Uhusiano kutoka TPDC, Augustino Kasale, alisema kuwa mradi unatarajiwa kupita katika mikoa nane kwa upande wa Tanzania na kutoa fursa za ajira zaidi ya 10,000. 

Alisema kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuzifahamu fursa za ajira zitakazo kuwepo ili waweze kuzichangamkia na kuongeza kipato chao. 

“Tunachokifanya kwa sasa kwa kushirikiana na serikali ya mkoa ni kuwaandaa wananchi wa Tanga katika kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotarajiwa kuwepo”, alisema Kasale. 

Alisema kuwa kuna fursa ya ajira za moja kwa moja na zile ajira za muda maalum ambazo zote hizo kama zitaweza kuchangamkiwa zitasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi mkoani humo. 

“Kuna fursa za ajira kama mahoteli, shughuli za usafirishaji wa mizigo na vifaa vya ujenzi, ulinzi, usafi huduma ya vyakula hizo ni sehemu ya ajira ambazo zinaweza kuhusisha mtu mmoja kwa mmoja”, alifafanua Kasale.

Kwa upande wa Mkoa wa Tanga umeanza maandalizi ya awali kwa ajili ya kupokea mradi huo ikiwemo kupima eneo litakalo tumika kwa ajili ya mradi huo pamoja na upanuzi wa bandari yake.

Naye Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema kuwa kwa sasa wapo kwenye jitihada za kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa mradi huo huku wakiwa na wajibu wa kufanya upanuzi wa bandari ya Tanga ili kujiandaa na kupokea shehena kubwa ya mzigo.

Alisema kuwa bandari ya Tanga inatarajiwa kupokea kiasi cha tani 250,000 za shehena ya mizigo ambavyo ni vifaa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo. 

“Yale tunayoweza kuyafanya sisi katika ngazi ya mkoa tayari mengi tumeyatekeleza kwa kiasi kikubwa tunachosubiri kwa sasa ni Marais pamoja na Mawaziri wan chi husika kuweza kutwambia lini ujenzi unaanza”amesema Mkuu wa mkoa huyo.

Anabainisha mmoja ya maeneo waliyokwisha fanya ushawishi ni pamoja na kuzungumza na wananchi kuhusu malipo ya fidia kwa wale ambao wanaweza kuathirika na ujenzi huo.

Alisema kwa kushirikina na timu ya wataalamu kutoka Kampuni ya Total wataendelea kufanya tathimini ya maeneo ambayo yanaweza kupitiwa na mradi ili kupata thamani halisi. 

“Tunajua kuna maeneo ambayo yataathirika moja kwa moja kwa mfano kwenye eneo hilo kuna skuli ya msingi ambayo ipo ndani ya eneo la mradi tayari tumeweza kuianisha na hivyo linahitajika kujengwa mahali pengine”, anabainisha RC Shigela.

Vile vile alisema kuwa wanaendelea na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa mradi huo kwa mkoa na Taifa kwa ujumla hivyo wandelee kutoa ushirikiano kwa serikali yao pamoja na wataalamu wakati wote wa utekelezaji wa wake.

Kuhusiana na fidia, Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa watahakikisha wanasimamia kwa ukaribu maswala ya fidia ili kuhakikisha kila mwananchi anaestahili kulipwa analipwa fidia kama fomu ya malipo inavyoelekeza.

“Tutahakikisha wananchi ambao mazao na nyumba zao zimeathiriwa wanatengewa maeneo mengine kwa haraka ili zoezi la ulipaji litakapoanza wasiweze kupata usumbuf”, alisema.

ENEO la machimbo ya mafuta mkoani Bunyoro nchini Uganda katika eneo la ziwa Albert (Picha kwa hisani ya mtandao)

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa kata ya Chongeleani Jijini Tanga wameiomba serikali kuimarisha ulinzi katika eneo ambalo linatarajiwa kuwekwa miundombinu ya mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi.

Mmoja wa wananchi aliejitambulisha kwa jina la Mumbi Twaha, alisema kuwa mradi huo ni mkubwa na unatarajiwa kutumia fedha nyingi hivyo ni vyema serikali ikaimarisha ulinzi mapema.

Alisema kuwa umarishaji wa ulinzi utasaidia kuzuiwa watu wenye nia mbaya ya kuhujumu mradi huo kwani kwa sasa kuna wageni wengi wanatembelea eneo hilo.

“Tunapokea wageni wengi na sisi kama wananchi hatuwezi kujua walio wazuri wala wale wenye nia mbaya hivyo tunaomba tujengewe kituo cha polisi katika kata yetu ili tuweze kuwa na uhakika wa ulinzi pamoja na usalama wetu”, alisema Twaha.

Nae Saleh Omar aliiambia makala haya kuwa licha ya kuweka vikundi vya doria wao kama wananchi lakini hofu yao wanaweza kuzidiwa nguvu na watu wenye nia ya kufanya hujuma.