NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
UJENZI wa Nyumba ya Makaazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika mtaa wa Pagali Chake Chake Pemba uliolenga kuondosha tatizo la makaazi kwa mtendaji huyo mkuu wa serikali unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Mshauri elekezi wa ujenzi huo kutoka Wakala wa Ujenzi Zanzibar aliyepo Kisiwani Pemba, Mhandisi Said Malik Said alisema ujenzi huo ulioanza mnamo mwaka 2018 tayari umeshafikia asilimia 97 na unakisiwa kugharimu shilingi bilioni 1.6.
Akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Pagali kukagua maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi huo, mshauri elekezi Said Malik Said alisema mafundi wako kwenye hatua za mwisho kupiga rangi.
Alisema miundombinu ya huduma za umeme, vipoza hewa, maji, barabara za ndani za makaazi hayo imeshakamilika na kinachomaliziwa katika mradi huo kwa hivi sasa ni ukamilishaji wa bustani ili kuyapamba makaazi hayo.
Mhandisi huyo alimueleza Balozi Seif kwamba licha ya mradi huo wa ujenzi kusimamiwa kitaalamu, bado ushauri wa wataalamu wa Wakala wa Ujenzi utazingatia kufuatilia mradi huo hadi pale watakapojiridhisha kwamba umekidhi vigezo vyote walivyoshauri na kuelekeza.
Balozi Seif ambaye aliambatana na viongozi kutoka katika ofisi yake alielezea faraja na kuridhika kwake na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi huo.
Balozi Seif alionyesha shauku ya kutaka kuyatumia makaazi hayo mara tu yatakapokamilika kabla ya kumaliza utumishi wake wa mtendaji mkuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakaofikia kikomo chake mara baada ya uchaguzi mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Miradi ya ujenzi wa majengo ya kudumu ya Ofisi za Serikali, makaazi ya viongozi na nyumba za kisasa kwa wananchi ni muendelezo wa falsafa ya Chama cha Afro Shirazy Party chini ya Muasisi wake Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.