NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali haitamvumilia mtu au kikundi cha watu kinachojihusisha na uvunjifu wa amani hasa katika kipindi hichi nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu.
Balozi Seif alieleza hayo wakati alipokwenda kumfariji na kumpa pole msanii mkongwe wa muziki wa tarab nchini Khamis Nyange Makame maarufu Profesa Gogo aliyelazwa kwa kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazimmoja.
Msanii huyo pamoja na wenziwe wawili walijeruhiwa kwa mapanga alfajiri ya Jumatatu huko kijijini kwao Kangagani kisiwani Pemba.
Makamu huyo alisema serikali itahakikisha inasimamia amani na utulivu uliopo kwa gharama yoyote hivyo wenye kutumia muda huu wa kampeni za kisiasa zinazoendelea kwa ajili ya kuchafua amani watashughulikiwa.
“Serikali itasimamia amani na utulivu uliopo nchini wakati huu wa kampeni zinazoendelea, wakati wa uchaguzi na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi”, alisema Balozi Seif.
Alifahamisha kuwa inasikitisha kuona kwamba jamii nzima ikiongozwa na viongozi wa dini wako kwenye ibada lakini wapo baadhi ya watu wanadiriki kuichezea amani hiyo kwa kushambulia na kujeruhi wengine.
“Jamii yote imejikita kudumisha amani hasa viongozi wa dini wakiwa mstari wa mbele katika jambo hilo, lakini wapo watu wanajaribu kuichezea amani tuliyonayo wakisahau kuwa hii ni tunu ya nchi yetu”, alisema.