NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema Zanzibar inajivunia kasi kubwa iliyopiga ya miradi ya kiuchumi na maendeleo ndani ya kipindi kifupi kutokana na usaidizi unaofanywa na taifa rafiki la China.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na balozi mdogo wa Jamhuri watu wa China aliyepo Zanzibar, Xie Xiaowu aliyefika ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar kuaga baada ya kumaliza muda wake wa miaka minne ya utumishi wa kidiplomasia hapa Zanzibar.

Alisema ipo miradi inayoshuhudiwa na wananchi na jumuiya za kimataifa ambayo tayari inaendelea kuwafaidisha watu wakati mingine ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.

Balozi Seif alisema Jamhuri ya Watu wa China ni mshirika wa karibu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambapo mara baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, nchi hiyo iliunga mkono miradi ya maendeleo katika taasisi mbali mbali.

Alibainisha kwamba ipo miradi iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili kama ujenzi wa kiwanda cha sukari, Mahonda, viwanda vya sigara na viatu Maruhubi, mashamba ya kilimo Upenja na Bambi sekta zilizotoa mchango mkubwa wa kitaalamu na ajira.

Makamu wa Pili, alimpongeza na kumshukuru Balozi huyo mdogo wa China kwa usimamizi wake mkubwa wa ushirikiano wa kidiplomasia uliosababisha kuibuka kwa miradi mingi ya kiuchumi na maendeleo.

Balozi Seif aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya sekta ya maji, ujenzi wa skuli za sekondari, huduma za afya hasa kipindi cha mripuko wa virusi vya corona.

Alisema China licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya bilioni 1.4 wanaohitaji huduma za msingi katika ustawi wao, lakini nchi hiyo inaiunga mkono Zanzibar katika kuona wananchi wa Zanzibar pia wanaendelea kudumisha ustawi wao.

Awali balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Xie Xie Xiaowu alisema anajisikia faraja kuona miradi mikubwa iliyoanzishwa katika kipindi chake imekamilika na mingine ikiwa katika hatua za mwisho.

Balozi Xiaowu alitolea mfano ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Abdullah Mzee iliyopo Mkoani Pemba, utanuzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Viwanja vya Michezo vya Mao Tse Tung, jengo la skuli iliyopo mtaa wa Mombasa, uwekaji wa taa za barabarani katika maeneo ya miji pamoja na usimamizi wa mafunzo ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar nchini China.

Alimhakikishia Makamu wa Pili wa Rais, kwamba licha ya kumaliza muda wake lakini uongozi mpya utakaoshika nafasi yake utaendelea kudumisha uhusiano uliopo.