NA KHAMISUU ABDALLAH
DAWA za kulevya zinazodaiwa kuwa ni majani makavu aina ya bangi kete saba zimemsababishia kijana mwenye umri wa miaka 20 kufikishwa mahakamani.
Mshitakiwa huyo ni Abdul malik Faraj Haji mkaazi wa mkaazi wa Jang’ombe wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ambae alifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa bila ya halali mshitakiwa huyo alipatikana na kifurushi cha karatasi ndani yake mkiwa na nyongo saba zilizofungwa kwenye karatasi nyeupe zikiwa ni majani makavu aina ya bangi yenye uzito wa gram 6.531 kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Kosa la kupatikana na kiwango kidogo cha dawa za kulevya ni kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa na kifungu cha 24 (a) cha sheria namba 1 ya mwaka 2019.
Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana na upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.
Mahakama ilikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21 mwaka huu na kuutaka upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.