NA KHAMISUU ABDALLAH

NYONGO nane za dawa za kulevya zimemsababishia Khalifa Ramadhan Puza, kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 35 mkaazi wa Shaurimoyo wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alifikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Mdhamini wa mahakama hiyo Mohammed Subeit.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Soud Said kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kupatikana na bangi kinyume na kifungu cha 16 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009 sheria za Zanzibar.

Hati hiyo ilidai kuwa Disemba 21 mwaka jana, saa 1:30 asubuhi huko Lumumba alipatikana na nyongo nane za dawa za kulevya aina bangi zenye uzito wa 8.726 g kitendo ambacho ni  kosa kisheria.

Aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Hakimu Subeit alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 15 mwaka huu na kuamuru kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Hakimu Subeit alisema dhamana ya mshitakiwa huyo ipo wazi ikiwa atajidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili ambao watamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha vitambulisho vyao vya mzanzibari mkaazi na barua za sheha wa shehia wanazoishi zinazoonesha namba ya nyumba.

Mshitakiwa huyo alishindwa kukamilisha masharti hayo na amepelekwa rumande hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.