NA NASRA MANZI
BARAZA la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni Zanzibar (BASSFU), limewataka wasanii wa maigizo, nyimbo na filamu, kuhamasisha amani na utulivu katika nchi kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu Mtendaji Baraza hilo Dk. Omar Abdalla Adam ofisini kwake Mwanakwerekwe Unguja.
Alisema kufanya hivyo kutawafanya wananchi kupata elimu zaidi na umuhimu wa amani, kwani wasanii wana nafasi kubwa ya kusikilizwa na jamii yao kupitia sanaa zao.
Hata hivyo alisema wasanii ndio kioo cha jamii, hivyo ni vyema kuandaa nyimbo ambazo zinakwenda sambamba na matukio na wakati wa jambo linapotokezea.
“Tunaona sasa uchaguzi unakaribia wasanii wetu watoe nyimbo zenye kwenda sambamba na matukio kwa kufuata maadili ” alisema
Aliwapongeza wasanii kwa kutojiweka nyuma na kujitokeza kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.
Aidha alisema wananchi wa Zanzibar wanahitaji uchaguzi wa amani, lakini pia kazi wanazozifanya lazima ziende sambamba na mazingira.