MUNICH, Ujerumani

MSIMU mpya wa ligi kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga ulianza bila ya mashabiki,juzi usiku huku bingwa mtetezi Bayern Munich akiinyeshia Schalke mvua ya mabao 8 – 0 katika mechi ya ufunguzi.

 Winga wa Ujerumani Leroy Sane alikuwa nyota wa mchezo na alifunga bao katika mechi yake ya kwanza ndani ya Bayern na Jamal Jamal Musiala mchezaji mwenye umri mdogo zaidi wa Bayern kuwahi kufunga bao akiwa na umri wa miaka 17

Serge Gnabry alifunga hat- trick na Sane akatoa usaidizi mara mbili kati ya mabao hayo. Mabao mengine yalifungwa na Leon Goretzka, Thomas Muller na Robert Lewandowski

Schalke haijashinda katika mechi 17 mfululizo wakati Bayern ikiendeleza rekodi yake ya kushinda mechi 22 mfulululizo.

Mipango ya Bayern kuwaruhusu mashabiki 7,500 kuhudhuria mechi hiyo dimbani ilifutwa na mamlaka za afya mjini Munich kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya corona.