NA MWAJUMA JUMA

CHAMA Cha Mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA), kimeshauriwa kuweka ligi moja ya mchezo huo, ambayo itakuwa na mizunguruko miwili kama ambavyo wenzao wa kisiwa cha Pemba wanavyofanya.

Ushauri huo umetolewa na kocha wa timu ya JKU ya mchezo huo Hija Khamis Rajab, alipokuwa akizungumza na gazeti hili  hivi karibuni mara baada ya kumalizika kwa ligi B ambapo JKU ilitwaa ubingwa.

Alisema Zanzibar ni Unguja na Pemba, ambapo Pemba imekuwa ikishiriki ligi moja tu ambayo haina kupanda na kushuka jambo ambalo linapaswa kufanyika Unguja.

Alisema  ligi hiyo ikiwa moja itakuwa ikichezwa mizunguruko miwili, ambapo mzunguuko mmoja utashirikisha timu zote na baadae watafute timu bora, ili kucheza mzunguruko wa pili  na kupatikana bingwa wa Zanzbar.

“Kweli tunacheza ligi B lakini timu zipo kidogo, je tunaziandaa vipi kwenda kucheza kule juu, kwa sababu timu imepata mechi kidogo tu lakini tukikutana wote kwa pamoja, tukacheza ligi wachezaji watapata mazoezi ya kutosha ya muda mrefu na kupatikana bingwa mzuri zaidi”, alisema.