NA ZAINAB ATUPAE

TIMU ya Black Sailors (Mabaharia Weusi) imerejea tena ligi kuu Soka ya Zanzibar, baada ya kumaliza mchezo wake wa mwisho kwa kuifunga Miembeni mabao 4-0, uwanja wa Mao Zedong B.

Kwa matokeo hayo Sailors imemaliza ligi kwa kufikisha pointi 51 huku wapinzani wao timu ya Uhamiaji ikimaliza ligi hiyo na pointi 49, baada ya kuwafunga Taifa ya Jang’ombe mabao 2-1 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Mao Zedong A.

Ligi Kuu Soka ya Zanzibar msimu ujao wa mwaka 2020-2021 itakuwa na jumla ya timu 12, moja pekee ikitokea kisiwani Pemba ambayo itatoka kwenye ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Pemba msimu huu wa mwaka 2019-2020 ambao bado unaendelea na timu 11 kutokea Kisiwani Unguja zitakuwa ni Mlandege, Zimamoto, JKU, KMKM, Mafunzo, KVZ, Kipanga, Polisi, Chuoni, Malindi na Black Sailors.

Akizungumzia mipango ya timu yake kocha mkuu wa timu hiyo Juma Awadhi, amesema wako katika mipango thabiti itakayosaidia kufanya vyema ligi kuu Zanzibar 2020-2021.

Alisema  miongoni mwa mipango yao ni kufanya usajili mzuri  katika nafasi zote ambazo zina mapungufu.

Alisema mbali na mpango huo, mpango mwengine ni kuitangaza timu yao kupitia vyombo vya habari, kwa lengo la kupata wadhamini watakaosaidia timu hiyo.