NA MARYAM HASSAN
WAFANYABIASHARA ya usafirishaji abiria kwa pikipiki (bodaboda) wametakiwa kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Wito huo umetolewa na Balozi wa usalama barabarani Farida Juma wakati akizungumza na wafanyabiashara hiyo wa Melitano Kwarara.
Alisema makosa mengi yanayotokea barabarani husababishwa na waendesha ‘bodaboda’ wanaokiuka sheria na kupelekea ajali.
“Ajali nyingi ni uzembe na upuuzaji wa sheria kwa kutaka kuwahi sehemu zenye abiria lakini mwisho wake mnasababisha ajali na kupoteza maisha au ulemavu wa kudumu jambo ambalo mnapaswa kujirekebisha,” alisema.
Wakati waendesha boda boda hao wakipatiwa elimu Balozi huyo aliambatana na ili kutia mkazo.
Akizungumza katika darasa hilo lililoendeshwa Askari polisi wa kituo cha polisi Fuoni, Koplo Haji Iddi Makame wa kikosi cha usalama barabarani aliwataka waendesha bodaboda hao kutii sheria ikiwa ni pamoja kuvaa kofia ngumu zenye kiwango vinavyokubalika.
Alifahamisha kuwa kofia hizo zinapaswa kufunika robo tatu ya kichwa na kuziba mdomo na kufungwa mkanda maalum pamoja na kukata leseni ili kuepuka kutozwa faini pindi wanapofikishwa mahakamani.
“Hii ni kazi kama kazi nyengine, hivyo nakushaurini mtekeleze yale mnayoambiwa pamoja na kufuata sheria zote za usalama barabarani zilizowekwa,” aliongeza koplo huyo na kuwahimiza kuvikatia bima vyombo vyao na kuvipasisha.
Aidha aliwahimiza kutoegesha vyombo vyao katika maeneo ya mpindo, kupakia abiria zaidi ya mmoja na kuendesha kwa mwendo kasi kupunguza ajali.
Akizungumza kwa niaba ya madereva Musaa Rajab Kombo aliahidi kutekeleza kwa vitendo yote yaliyofundishwa na kulishauri jeshi hilo kutoa elimu hiyo mara kwa mara.
“Mkifanya hivyo mtakuwa mnatumbusha na kupelekea kupungua kwa matukio ya ajali za mara kwa mara lakini pia tunaahidi kutoa elimu hii kwa wenzetu ambao hawakuipata,” alisema.