NA HAFSA GOLO

BODI ya Ushauri ya Wakala na Vipimo imesema itasimamia kwa ufasaha na weledi sheria mpya ya wakala wa vipimo ili kumlinda mtumiaji sambamba na kuhakikisha vipimo vyote vinapima kwa usahihi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala huo Mohammed Mwalim Simai, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili huko ofisini kwake Migombani kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo namba 6 ya mwaka 2020.

Alisema atahakikisha kunakuwa na haki na uhuru juu ya vipimo vyote na hatomvumilia mtu yoyote atakaekiuka masharti na maelekezo ya sheria hiyo ambayo ina manufaa makubwa kwa taifa na wananchi kwa jumla.

Aidha alisema, hatua hiyo itakuwa sambamba na udhibiti wa bidhaa wenye kufuata masharti ya kitaalamu.

Alisema, zoezi hilo litazingatia umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo kwenye maeneo tofauti katika maisha ya kila siku.

Alifahamisha miongoni mwa utekelezaji utakaozingatiwa ni pamoja na kuhakikisha masuala ya vipimo yanachukua nafasi kubwa kwenye mipango ya kisayansi, viwanda na maendeleo ya teknolojia.

Alibainisha msingi mkuu wa maendeleo ya kisayansi na viwanda ni vipimo, ambapo kukosekana kwake kunapelekea uzalishaji duni pamoja na udhibiti bora kwenye viwanda.

Akizungumzia kuhusu vipimo na uwekezaji alisema, atahakikisha kunakuwa na miundombinu rafiki ambayo itamshawishi muwekezaji aweze kuwekeza nchini ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa vipimo ambavyo udhibiti dhidi ya uzito mkubwa wa gari na mizigo inaoweza kuathiri nchi.

Pia wataangalia ubora wa bidhaa pamoja na huduma zitolewazo na muwekezaji kwenda kwa wateja wake utakaohitaji nyezo muhimu ambapo kwanza kutakuwa na mfumo mzuri wa kivipimo utakaomhakikishia matokeo sahihi.

Alisema mfumo huo utatoa matokeo ambayo yatapelekea huduma za uhakika wa bidhaa bora pamoja na huduma zitolewazo kwa wateja.