NA HAFSA GOLO

BODI ya Ushauri ya  Wakala na Vipimo imetakiwa kuepuka kufanyakazi kwa ubaguzi na kuweka  maslahi binafsi mbele ili kutimiza malengo yaliokusudiwa.

Waziri  wa Biashara na Viwanda, Balozi  Amina Salum Ali, alitoa agizo hilo wakati akizindua bodi hiyo katika  hafla iliyofanyiwa ukumbi wa wizara hiyo Migombani.

Alisema iwapo watendaji wa bodi hiyo watafata sheria, maadili, na miongozo ya majukumu ya kazi zao itasaidia kuondosha urasimu wa kiutendaji na kuleta mafanikio ya haraka ya ndani ya bodi hiyo.

Wazir Amina alisema suala la uadilifu, mashirikiano na kubadilishana uzoefu kwa kutafuta fursa zaidi za kujifunza huku wakiwatumia vijana waliosomea fani hiyo chombo hicho upo uwezekano wa kuleta mafanikio makubwa serikalini hasa ikizingatiwa kutokana na umuhimu wake.

Alisema kutungwa kwa sheria ya Wakala wa Vipimo namba 6 ya mwaka 2020 ni miongoni mwa  hatua za mageuzi zilizofanyika ndani ya Wizara ya Biashara na Viwanda kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza biashara.

Alisema lengo jengine la kutungwa kwa sheria hiyo ni pamoja na   kuondosha urasimu katika utoaji wa huduma na kuweka ushindani halali wa kibiashara pamoja na kumlinda mlaji.

Alifahamisha kuundwa kwa wakala huo ni hatua muhimu  katika kuimarisha mazingira ya kibiashara hapa  Zanzibar sambamba na mkombozi kwa wananchi na wazalishaji katika viwanda vya ndani katika kuvifanya viendane na dhamira ya serikali ya Tanzania ya viwanda.

“Ujio wa sheria mpya ya Wakala wa Vipimo ni mkombozi si kwa wananchi pekee ambao watakuwa na uhakika kwenye vipimo wanavyotumiwa katika miamala ya kibiashara bali hata kwa wazalishaji katika viwanda vyetu vya ndani na kuvifanya viendane na kauli mbiu ya “Tanzania ya Viwanda”,alisema.