Afunguka mengi kuhusu mahusiano yake 

FLOYD Mayweather ni mwanamichezo aliyejijengea umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake kwenye masumbwi. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 41 anachukuliwa kama mmoja wa mabondia wazuri waliowahi kutokea ulimwenguni.

Uwezo wake ulingoni hakuna anayeweza kuutilia shaka kwani katika mapigano 50 ya kulipwa aliyoshuka ulingoni hadi anatangaza kustaafu mwaka 2017, hajawahi kupigwa hata pambano moja.

Katika jumla ya mapambano 50, Mayweather amewapiga wapinzani wake 27 ndani ya muda uliopangwa kumaliza pambano kumalizika ambapo kwa maana halisi ya mchezo huo amewapiga kwa ‘knockout’.

Pambano la mwisho baina ya Mayweather na Conor McGregor ndilo alilotangaza kuhitimisha rasmi kuingia ulingoni, ambapoa wali pia aliwahi kukaririwa kuwa atastaafu ndondi baada ya kumtwanga Manny Pacquiao.

Sitaki nimuangalie bondia huyu kwenye ulingo wa masumbwi katika makala haya nitajaribu kuangalia baadhi ya vituko vya mambo binafsi ya Mayweather kijana mwenye misifa ya kupunda fedha kutokana na matanuzi.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, kijana huyo amejikusnayia utajiri mkubwa ambapo hadi mwaka huu alikuwa na utajiri wa dola milioni 400 ambazo zimetulia benki.

Ndondi ndio mchezo ulipatia fedha hizo nyingi ambapo pambano kati ya na Mfilipino Manny Pacquiao lililopiganwa mwaka 2015, lilimuwezesha kumuingizia kiasi cha dola milioni 250, huku lile McGregor likimuingizia dola milioni 100.

Mayweather si kijana mwenye kuficha utajiri alionao, kwani mara nyingi hujipiga picha na kuzianika kwenye mitandao ya kijamii kionyesha minoti kwa minoti ya midola.

Video na picha anazorusha akionyesha misifa ya kuwa na mkwanja mrefu imekuwa ikiwaudhidi baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii huku wakutoa maeneo kadhaa wa kadhaa.

Kwenye moja ya video, Mayweather alisema kwamba hajui kwanini watu wana chukia namna anavyotumia pesa zake alizozitengeneza na kuzipata kwa juhudi zake.

“Hizi pesa ninazotumia nimezitafuta kwa juhudi zangu, sijamkopa mtu na kumuibia sasa kwanini watu wachukie”, alihojia bondia huyo.

Mara nyingi Mayweather, hupiga picha sehemu tofauti akiwa na mibunda ya minoti huku akitwanga raha na kula bata akiwa na warembo wenye sura na mavuto kwa kiwango cha juu kabisa.

Hivi karibuni gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza lilichapisha makala fupi inayomnakili bondia huyo akielezea masuala yake ya mahusiano ya kimapenzi.

Mayweather alisema ana mahusiano na wanawake saba na kwamba wote anawahudumia kama inavyotakiwa bila ya matatizo yoyote.

Wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Awkward Puppets, kwanini awe na idadi hiyo ya wanawake? Mayweather alisema kuishi na mwanamke mmoja ni sawa na kuwa huna mwanamke.

“Kuishi na mwanamke mmoja ni sawa na kuwa huna mwenza”,alisema Mayweather bila ya kufafanua kiundani alikuwa na maana gani wakati dini yake ya kikiristo anasisitiza mke mmoja.

“Mara nyingi wachumba zangu huwa nasafiri nao, tunapata chakula pamoja, kuwa na mwanamke mmoja ni kukaribua kuwa huna”,alisisitiza.

Kuhusu suala la ndoa alisema hana haraka sana kufunga ndoa kwasababu unapooa suala la kuachana na mke nalo halipo mbali.

“Ukioa basi hata kuachana nako hakuko mbali”,alisema.

Mayweather amekuwa akihusishwa kuwa na uhusiano na warembo kadhaa wakiwemo mwanadada kutoka nchini Uingereza, Rmarni Ellis, Abi Clarke, Yahaira Vianne Ochoa, Melissa Brim na Doralie Medina.

Kuhusu utajiri wake alionao alisema ana kama dola milioni 200 au 300 ambazo ameziweka kwenye akaunti katika benki mbalimbali zilizopo katika mji wa Las Vegas.

Bondia huyo alisema ana miliki gari 25 za kifahari za aina tafauti tofauti.

Kitu chengine alichokisema kwenye mahojiano ni kwamba hatashuka tena ulingoni na kwamba pambano lake la Conor McGregor ndilo la mwisho katika maisha yake na kamwe hatoshuka ulingoni.

“Nilisema kuwa pambano la Conor McGregor ndilo la mwisho kwangu, nataka nirejee tena kusema kuwa sitashuka tena ulingoni kupigana ngumi za kulipwa”, alisema Mayweather.

Baada ya pambano lake na McGregor, alijipongeza kwa kushinda pambano hilp kwa kununua jumba la kifahari huko Beverly Hills nchini Marekani.

Pambano hilo lilimuingizia Mayweather zaidi ya fedha za kitanzania shilingi bilioni 225, na hakupoteza muda kuzitumia fedha hizo kwa kunua nyumba.

Jumba hilo amelinunua kwa shilingi bilioni 60 za kitanzania. Mayweather pia ametumia zaidi ya bilioni moja za kitanzania kwa ajili ya kuliweka sawa ili liweze kukalika vizuri zaidi.

Jumba hilo lina ukumbi mkubwa wa kuangalia sinema, vyumba vya wageni, na sehemu nzuri ya kustarehe nje ikiwemo sehemu nzuri ya kuogelea.