LONDON, England
NYOTA wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, ameitahadharisha Manchester United kwamba safu yao mpya ya viungo watatu itawaletea matatizo makubwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
United imefanya usajili mmoja tu dirisha hili la majira ya kiangazi ilipomsajili, Donny van de Beek kutoka Ajax.
Raia huyo wa Uholanzi ambaye ni kiungo amekwenda kuongeza nguvu kwenye eneo la kati kati ya uwanja ya kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer na uwezo wake ni kucheza nambari 6, 8 au 10.
Kutokana na kuwepo kwa Bruno Fernandes na Paul Pogba, viungo hao watatu wanaonekana watakuwa wakiunda kombinesheni inayotazamwa itakuwa tishio kwenye ligi.
Hata hivyo, Carragher, anaamini hali hiyo itawafanya United kujielekeza zaidi kwenye mashambulizi hali ambayo itawaweka kwenye hatari ya kufanyiwa mashambulizi ya kushtukiza.
Hivyo, alisema, kuchezesha viungo wote watatu haoni kama itakuwa sahihi na huenda ikawagahrimu.
United ilikumbana na kipigo cha magoli 3-1 mbele ya Crystal Palace kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England, wakifungwa mara mbili na Wilfried Zaha na Jordan Ayew.
“Crystal ni wazuri kwenye mashambulizi ya kushtukiza, lakini, United bado hawajakutana na timu yenye ubora mkubwa uwanjani”, alisema, Carragher.
“Kuwatumia viungo hawa watatu kwa pamoja kutaifanya United kuwa kwenye matatizo katika kuzidhibiti timu zinazocheza soka la mashambulizi ya kushtukiza”.(Goal).