NA IS-HAKA OMAR
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa hadhara wa kampeni uwanja wa skuli ya Nungwi.
Akizungumzia maandalizi ya mkutano huo katibu msaidizi mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Daud Ismail Juma, alisema maandalizi ya mkutano huo tayari yamekamilika.
Alisema katika mkutano huo Dk. Shein, atapata kuelezea kwa kina sera, mikakati na muelekeo wa CCM pamoja na mambo ya maendeleo yaliyotekelezwa kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Alieleza kuwa Makamu Mwenyekiti huyo atawatambulisha na kuwaombea kura wagombea wa ngazi za ubunge, uwakilishi na udiwani na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Mwinyi, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan.
Katibu huyo alisema Makamu Mwenyekiti wa CCM atawakabidhi wagombea hao ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ambayo ni muongozo na nyenzo ya kufanyia kazi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katibu huyo alifafanua kwamba kupitia mkutano huo mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM atafafanua namna atakavyosimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2020 na kuvieleza vipaumbele vya uongozi wake.
Daud, aliwaomba wanachama wa Chama cha Mapinduzi, makada na wananchi kwa ujumla kufika katika mkutano huo wa hadhara kusikiliza sera za Chama zinazoendana na matarajio ya wananchi wengi wanaopenda maendeleo ya nchi na ustawi wa kijamii.
Alisema viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi watahudhuria mkutano huo wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Sadalla.
Alieleza kuwa mkutano huo utapambwa na wasanii kutoka Zanzibar wakiwemo wasanii wa kizazi kipya, taarab, band na burudani mbalimbali zitazowavutia wananchi.