LONDON, England
KLABU ya Chelsea imeingia kwenye orodha ya vigogo vya England vilivyofikisha zaidi ya pointi 2000, tangu kuanzishwa kwa ligi kuu ya nchi hiyo Februari 20 mwaka 1992.

Miamba hiyo imefikisha pointi hizo baada ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya England msimu huu dhidi ya Brighton & Hove Albion juzi.

Hata hivyo, klabu hiyo ya jijini London imetanguliwa na Manchester United wanaoongoza kwenye orodha hiyo (2,231), ikifuatiwa na Arsenal (2,014), na ‘The Blues’ wanashika nafasi ya tatu.

Lakini katika orodha hiyo klabu hizo tatu ndizo zimefikisha pointi 2000 na zaidi, na zinazofuatia bado zipo chini ya alama hizo.

Orodha ya vigogo vyengine ambavyo vina pointi nyingi zaidi tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo miaka 28 iliyopita ni pamoja na Liverpool (1,951), Tottenham Hotspurs (1,654), Everton (1,479), Manchester City (1,450) na Newcastle United (1,319).