LONDON,England

IMERIPOTIWA kuwa klabu ya Chelsea ipo tayari kumtoa kipa wao namba moja, Kepa Arrizabalaga kwa mkopo baada ya kumpata mbadala wake ambaye ni Edouard Mendy kutoka klabu ya Rennes.

Frank Lampard, Kocha Mkuu wa Chelsea amempa dili la miaka mitano Mendy kwa kiasi cha Euro milioni 22.

Kepa amekuwa hana furaha baada ya kufanya makosa wikiendi iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu England wakati wakipoteza kwa kufungwa mabao mawili ambayo yalifungwa na Msenegal, Sadio Mane na kuwafanya wayeyushe pointi tatu Uwanja wa Stamford Bridge.

Inaelezwa kuwa Lampard amepoteza matumaini kwa Kepa licha ya kutoweka wazi kwamba hana imani naye na sababu ya kutaka kumtoa kwa mkopo ni kufanya aweze kuwa imara huko atakokwenda kwa kuwa hatakuwa na nafasi ndani ya kikosi cha Chelsea kwa wakati ujao.

 Gary Neville mchezaji wa zamani wa Manchester United na Jamie Carragher mchezaji wa zamani wa Liverpool wamesema kuwa Chelsea haina nafasi ya kutwaa taji la Ligi Kuu England ikiwa itamtumia Kepa langoni kutokana na makosa yake kujirudia.