NA NIZAR VISRAM

KATIKA makala yangu ya mwisho tumeona kuwa mauaji ya Mmarekani mweusi, George Floys halikuwa tukio la pekee bali ni moja kati ya matukio mengi ya polisi kuwaua raia wa Marekani wenye asili ya Afrika.

Na mara zote kumekuwepo na maandamano ya wananchi waliokasirika na kudai mabadiliko.

Tofauti ni kuwa mara hii maandamanao yameibuka kote duniani. Na kote wananchi wanajiuliza masuali ya kimsingi. Kwa mfano kuna mamia ya sanamu za watawala waliokuwa wabaguzi na walikuwa wanamiliki watumwa. Je sanamu hizi ziendelee “kupamba” miji yetu?

Baadhi ya sanamu hizi zimeng’olewa na kutoswa baharini. Inawezekana baada ya yote haya kumalizika hali ikaendelea kama kawaida. Mauaji mengine yatafanyika na wananchi wataandamana tena. Hii ndio hali ya Marekani ambayo imekuweko kwa muda mrefu.

Kwa mfano, polisi huwa wanatumia bastola inayoitwa Taser. Wanadai kuwa silaha hii inajeruhi tu kwa kutumia umeme na wala haiui. Lakini shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa hadi mwishoni mwa 2018 raia wasiopungua 1,081 wameuawa kutokana na silaha hii. Tangu wakati huo idadi hiyo imeongezeka. 

Asilimia 32 ya waliouliwa kwa Taser ni weusi na asilimia 29 ni weupe. Ikumbukwe kuwa nchini Marekani raia weusi idadi yao ni asilimia 14 na weupe ni asilimia 60.  Maana yake Taser inatumiwa zaidi dhidi ya weusi kuliko weupe. Hii ni ishara tosha kuwa kuna ubaguzi wa rangi.

Ni vizuri ikaeleweka kuwa ubaguzi wa rangi na mauaji ya raia weusi nchini Marekani si suala la polisi wachache kuwa wabaguzi, wala si sula la samaki mmoja kuharibika. Ubaguzi na udhalilishaji haujaanza jana wala juzi bali umekuwepo kwa karne nyingi nchini Marekani.

Ubaguzi nchini Marekani umeota mizizi katika historia ya nchi hiyo. Una historia ndefu tangu enzi za utumwa wakati mamilioni ya Waafrika walipotekwa nyara na kusafirishwa hadi Marekani ambako wakafanyishwa kazi katika mashamba ya pamba.

Na hata baada ya kumalizika kwa utumwa, huo haukuwa mwisho wa ubaguzi na mauaji ya weusi. Kwa muda mrefu kumekuweko na kikundi cha makaburu kinachojiita KKK (Ku Klux Klan). Hawa wanaamini kuwa Marekani ni nchi ya wazungu na weusi ni watu duni wasio na haki za kiraia.

Wasiwasi wao mkubwa ni kuwa itakapofika mwaka 2043 idadi ya weupe walio wengi hivi sasa watazidiwa na wasio weupe. Raia wenye asili ya Amerika kusini (Latino) walio milioni 53 hivi sasa watazidi na kufikia milioni 128, Waamerika weusi walio milioni 41 hivi sasa watafikia 62 milioni.

Ndipo KKK wamekuwa wakipinga vikali na kwa nguvu kuwepo kwa weusi nchini Marekani. Mkuu wao alikuwa David Duke ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican na aliwahi hata kuchaguliwa kama mbunge. Katika uchaguzi wa 2016 alimpigia debe Rais Trump.

Katika hali kama hii ndipo tunona mwaka 1967 yalizuka machafuko mjini Detroit na weusi 33 wakauawa kwa kupigwa risasi. Serikali ikaunda tume ya Kerner ili kufanya uchunguzi na kujua chanzo chake. Katika ripoti yake tume ikasema machafuko yametokana na mfumo wa kibaguzi.

Ripoti ya Kerner ikaendelea: “Kuna kitu ambacho Waamerika weupe wangali hawaelewi, nacho ni kuwa kuna mpasuko katika jamii ambayo imegawanyika katika vipande viwili. Raia weusi wanaishi katika maeneo duni yanayojulikana kama geto. Hii imetokanana na mfumo ulioundwa na jamii ya weupe na mfumo huu unaendelezwa na kulindwa na weupe.”

Tume ikaeleza kuwa mfumo wa geto umetokana na matabaka ya wenye nacho na wasio nacho,  matabaka ambayo yameanza tangu enzi za utumwa nchini Marekani.

Tume ikapendekeza kuwa badala ya raia weusi kutengwa katika geto, kinachotakiwa ni kuinua hali ya maisha katika maeneo yao. Kwa njia hii utengano uliopo utavunjika na watu watakuwa na mawazo ya utengamano.  

Hakuna kilichofanyika baada ya ripoti hiyo ya Kerner. Ukweli ni kuwa tume kama hizo zimekuwepo zaidi ya miaka 150 iliyopita. Kila wakati serikali hutakiwa kuwekeza katika maendeleo na ustawi wa wananchi masikini.

Badala yake serikali zote, bila kujali zinaongozwa na chama cha Republican au Democrat, zimekuwa zikipunguza bajeti zake katika huduma za kijamii. Badala yake huongeza bajeti ya majeshi.

Serikali hizo zimekuwa zikiruhusu makampuni kuwapangia wafanyakazi wao mishahara duni bila ya kujali athari yake katika maisha ya wafanyakazi na familia zao.

Na walioathirika zaidi ni wafanyakazi weusi. Pia tunaona mwaka 2008 uchumi ulipoporomoka nchini Marekani, raia weusi ndio walioathirika zaidi kwa kupoteza hata nyumba walimokuwa wakiishi.

Mwaka 2013 utafiti uliofanywa na shirika la Pew Research uligundua kuwa, kwa wastani, akiba ya familia ya weupe ni mara 13 zaidi kuliko ile ya familia ya weusi. Utafiti pia ulionyesha kuwa tofauti hii inazidi kuongezeka.

Hivi sasa kuna huu ugonjwa wa corona ulioibuka hivi karibuni na kuua zaidi ya watu 133,000 nchini Marekani. Tarakimu inaonyesha kuwa raia weusi wanaambukizwa zaidi kuliko weupe.

Kuna watakaojiuliza, iweje hali hii iendelee zaidi ya miaka 155 baada ya kumalizika kwa utumwa huko Marekani. Ni sawa na kuuliza inakuaje baada ya ukoloni kumalizika barani Afrika unyonyaji unaendelea chini ya ukoloni mambo-leo.

Waingereza walianza kuwashika Waafrika kama watumwa kutoka Afrika magharibi na kuwasafirisha hadi Marekani ililokuwa koloni lao. Walianza biashara hiyo tangu karne ya 17 kabla hata kuanza kwa ukoloni.

Mwaka 1672 mfalme wa Uingereza, Charles wa pili alitoa kibali cha biashara ya utumwa kwa kampuni pekee ya Royal African Company. Hakuna kampuni nyengine iliyopewa kibali hicho cha kuwanunua watumwa kutoka Afrika magharibi na kuwapeleka Marekani.

Ndipo kwa muda wa karne mbili Waafrika, wanaume kwa wanawake, wakubwa kwa wadogo, waliibwa, wakafungwa minyororo na kuuzwa nchini Marekani. Inasemekana kati ya watumwa milioni 12 waliosafirishwa kutoka Afrika, milioni 1.5 walikufa wakiwa njiani kutokana na njaa na mateso.

Mapema karne ya 19 watumwa wengi nchini Marekani wakamudu kujitoa kutoka makucha ya utumwa. Hii haikuwa rahisi kwani wamiliki wa watumwa katika majimbo ya kusini walikataa kuwaachia. Ndipo wakakimbilia kaskazini katika majimbo kama New York, Boston na Philadelphia.

Hapa wakakumbana na mashambulizi ya walowezi waliokuwa wakihamia Marekani kwa wingi kutoka Ujerumani, Ireland, Uingereza, Italia, Poland na Urusi. Katika karne ya 19 kukawa na magenge ya walowezi weupe wakiwashambulia weusi na kuwaua. Serikali ikawalinda weupe.

Kwa mfano, meya wa Cincinatti (Ohio) aliamrisha kukamatwa kwa mamia ya weusi na kuwasweka jela. Ni mzungu mmoja tu alikamatwa.  Hali hii ikazidi kupamba moto baada ya kupitishwa kwa sheria zilizoitwa Jim Crow ziliyotoa ruksa rasmi kwa weupe kuwabagua weusi. 

Ndipo mwaka 1919 weusi 200 waliuliwa mjini Elaine (Arkansas). Mjini Chicago kijana mweusi aliyediriki kutembelea fukwe ya bahari alivamiwa akapigwa mawe na kutupwa katika ziwa la Michigan.

Baada ya hapo kukazuka mapigano makali katika Chicago na weusi 23 na weupe 15 wakafa. Kaya 1,000 za weusi wakachomewa nyumba zao.

Mchungaji Jeremiah Wright alipokuwa akitoa mhadhara katika chuo kikuu cha Howard jijini Washington mnamo 2006 alisema: “Nchi hii iliasisiwa kibaguzi na inaendelea kutawaliwa kibaguzi. Tunaendelea kuamini kuwa mtu mweupe kimaumbile ni bora kuliko mtu mweusi, zaidi kuliko tunavyomuamini Mungu”.

Wright, aliyekuwa mshauri wa kiroho wa rais mstaafu Barrack Obama, pia alisema Marekani badala ya kutumia nguvu zake kupigana vita duniani, ni vizuri tukapigana vita ndani ya nchi yetu dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa kitabaka.

Akaongeza kuwa kinachotakiwa ni kuleta mabadiliko ya kimsingi kwa kutumia bajeti. Alitoa mfano wa aliyekuwa rais George W Bush alipotoa “zawadi” kwa matajiri kwa kuwasamehe kodi ya dola trilioni 1.3, badala ya kutumia kodi hizo za wananchi katika matibabu na elimu kwa jamii masikini.

Mawazo kama haya yalitolewa zamani na mwanaharakati mweusi, Malcolm X wakati Rais Kennedy wa Marekani alipouliwa. Alisema mauaji hayo ni matokeo ya chuki – “Ni chuki ambayo Marekani imeieneza duniani kote na sasa inaturudia nyumbani”.

nizar1941@gmail.co 0658-010308