ZASPOTI

UMEWAHI kuhisi unaachwa na mtu unayetarajia kumuoa au kuolewa nae? Umewahi kujisikia vibaya mwenzi wako akizungumza na mtu mwengine hata kama hukuwa na ujasiri wa kumwambia? Umewahi kumchukia mtu na hata kupambana nae kwa siri au wazi sababu tu umehisi anahatarisha uhusiano wako? Kama lolote kati ya hilo linaelezea hali yako, basi makala haya yanakuhusu.


Najua wapo,tena wengi, wanaoamini ni vigumu kutenganisha hisia za wivu na mapenzi.Wanaamini huwezi kumpenda mtu bila kumwonea wivu.
Lakini ni hisia hizo hizo za wivu ndio zimekuwa chanzo cha maumivu ya moyo, majeraha, talaka na hata vifo vya watu tunaoambiwa ni wapenzi.
Haya hayawezi kuwa matokeo ya upendo,wivu umesababisha watu wasiwe na amani na mahusiano yao.


Wivu umesababisha watu wawe na hasira, ghadhabu na uchungu, wakati mwingi, kwa mambo yasiyokuwepo.
Wapo waliofikia kugombana na watu wasiohusika kwa sababu tu wanahisi kuingiliwa kwenye uhusiano. Wivu si hisia zinazoweza kuleta faida hata kama wengi wanaamini hivyo.

WIVU UGONJWA WA NAFSI ISIYOJIAMINI

Kuhisi mtu unayempenda anaweza kuwa na hisia za kimapenzi na mtu mwengine sio jambo la kujivunia. Kutomuamini mpenzi uliyenaye na kuhisi kuna mtu mwengine anahatarisha uhusiano wenu haiwezi kuwa afya ya mahusiano.


Ingawa wakati mwengine hisia hizi huwa sahihi, wakati mwingi huwa ni hisia tu zisizokuwepo. Ni hisia za kutokujisikia salama na kutojiamini.
Uhusiano wenye tishio la wivu, kuhisiana, kupekuana, na kadhalika, hutegemea namna gani mtu aliye kwenye mahusiano asivyojiamini kwa maana ya kuwa na nafsi isiyotulia kumwezesha kujiamini na kuwaamini wengine.


Malezi ndio msingi wa kutojiamini si kazi nyepesi kwa mwenzi aliyekuzwa bila kujiamini kujisikia salama nafsini,hajiamini na hawaamini wengine.
Watafiti wengine wanakubaliana kwamba wivu ni matokeo ya imani batili kuhusu mapenzi na mahusiano, wivu ni imani.


Ukweli ni kwamba unapoamini hakuna mtu anaweza kuwa mwaminifu kwenye ndoa hata ufanyeje,unajenga matarajio yanayoweza kutengeneza uhalisia usiokuwepo.
Imani kuwa hakuna mtu anayeweza kuwa mwaminifu huathiri mtazamo wako na hivyo huwezi kumwamini mkeo anaposafiri kikazi kwa siku kadhaa.


Unajenga hofu unaposikia mumeo anakwenda kazini kwa zamu ya usiku.Na ubaya wa imani hizi zinazojengeka kwenye ufahamu humtafuna mtu ndani kwa ndani hivyo hata usiposema ulivyo na wasiwasi, lakini unajua unavyopata tabu moyoni kwa kujua lolote linawezekana kutokea. Hakuna uhusiano wowote unaweza kuleta utimilifu wa furaha inayotarajiwa katika mazingira haya ya hofu na mashaka.

WIVU NA MAPENZI HAVIENDANI PAMOJA

Hisia za wivu zikishakomaa ndani kwa ndani huhamia kwenye hatua inayoweza kuonekana wazi.
Hapa tunasema hisia zinahama kutoka kuwa mtazamo na imani hasi na kuwa tabia.
Katika hatua hii mtu huanza kuchukua hatua za kujihami katika kukabiliana na tishio linalohisiwa.


Hapa tunazungumzia mbinu za kuanza kuchunguza mwenendo wa mwenzako kwa siri.Kuanza kumfuatilia kujua mambo yake ya faragha. Kuanza kuonesha wasiwasi wako waziwazi.
Katika hatua hii mtu huanza kupekua simu kwa siri,kupekua kompyuta kujua kurasa zisizoperuziwa au hata kuuliza kwa wengine mwenendo wa mwenzake.


Katika hatua hii, kadhalika, mtu huanza kufanya majaribio ya kupambana na kile kinachohisiwa kutishia uhusiano wake,huanza kuthubutu kuanza kuwapigia simu watu anaohisi ndio tatizo.
Mchanganyiko wa hasira wasiwasi, hofu na uchungu humfanya adhamirie kupambana na watu anaowahisi iwe kwa maneno au hata kwa matumizi ya nguvu.


Huwezi kumpenda mtu kwa dhati wakati huo huo ukimfuatilia kwa karibu kwa matarajio ya kukusanya ushahidi usijenga mahusiano yenu.
Wivu, kama tulivyoona ni matokeo ya kutokujiamini,ni udhaifu, Na kwa hakika huwezi kupenda kama wewe mwenyewe hujiamini.
Tafiti zimethibitisha hivyo kwamba kadri unavyompenda mwenzi wako, ndivyo inavyokuwa vigumu kuhisi kuibiwa.

TUNAWEZA KUKABILIANA NA WIVU

Unapopata hisia za wivu, jambo la kwanza la kufahamu ni kwamba bado hujaweza kujiamini ipasavyo.
Na kuna ukweli fulani kwamba ni mara chache unaweza kumbadilisha mwenzako.Kumbe kwa kutokujiamini na kujipenda, unajiwekea mazingira ya kuteseka unapoingia kwenye mahusiano.
Kwa lugha rahisi kabisa, hisia za wivu maana yake ni kutoamini watu Una mashaka na tabia za watu.
Unaamini uko sahihi, wengine wanakosea badilika,tafuta msaada uweze kuwaamini watu. Itakusaidia kuepuka kuteseka kwa mambo yasiyokuwepo kwa sababu tu huwezi kuwaamini watu.Kutoamini, ndiyo wivu wenyewe.


Ni kweli kuwa wakati mwengine hisia za wivu huwa hisia za hali iliyopo. Kwamba ni kweli yupo mtu wa tatu katika mahusiano yenu.
Kama mwanadamu unajisikia vibaya,lakini dawa si wivu wa kiwango cha kupambana na mshindani wako.
Katika mazingira hayo, wakati mwengine tatizo huwa ni wewe.Ndio huenda hujalipa gharama ya kumfanya mpenzi wako ajisikie kupendwa na kuthaminiwa.
Huenda umemfanya ajisikie kutumika kama daraja la mtu kufikia malengo mengine ya kimaisha.


Badilisha mtazamo wako,tafuta msaada wa kukufanya ujisikie mwenye wajibu wa kuleta mabadiliko kwenye mahusiano yako,wivu haukusaidii kutatua matatizo yako.
Wivu usikufanye upambane na mtu asiyehusika,Hasira ni kiburi,hasira, Itakugharimu kukarabati mahusiano kwa kuongeza duara la mapambano na mtu wa tatu.
Pambana na mwenzi wako kwa kumpa haki yake,kama una hakika analo tatizo la kuvutwa na vya nje, kabiliana naye abadilike.


Tafuteni msaada wa kitaalamu kushughulikia mahusiano yenu.Hamna haja ya kupambana na mtu wa tatu ambaye kimsingi mmemkaribisha wenyewe.
Wivu ni sumu mbaya katika mahusiano,unapojisikia hatari ya kumpoteza mpenzi wako, unapojisikia unatumia nguvu nyingi kuliko anazotumia yeye, maana yake ni kwamba bado hujampenda.


Ni hatari ya hisia zako, na za mwenzako,unajeruhi hisia zao mara nyingi kwa jambo lisilokuwepo.
Unajikuta unachukua hatua zinazoongeza majeraha hata baada ya kushughulikia tatizo lenu.
Kabla hujafanya maamuzi ya kuhusiana na mtu, jitathimini, Jichunguze mwenyewe kwanza Je, unajiamini? Unaamini wengine? Unafikiri nini kuhusu kupenda na kupendwa? Je, mahusiano ni kulipa gharama au kutarajia kutendewa? Kama huna hakika, tafuta msaada ndipo uweze kuingia kwenye uhusiano.