BEIJING, CHINA

SERIKALI ya China inatarajia kuzalisha zaidi ya chanjo milioni 600 za virusi vya Corona hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Ofisa mwandamizi wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia ya China alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa chanjo nne kati ya kumi na moja zenye uwezo wa kutumika zinazoendelezwa nchini China, zipo katika awamu ya mwisho ya majaribio ya kitabibu na kuwa majaribio hayo yanaendelea vyema.

Ofisa huyo Wu Yuanbin, alisema awamu za majaribio ya mwisho zinafanyika nje ya China pia.

Alisema chanjo mbili kati ya nne zenye uwezo, zinazoendelezwa na shirika linalodhaminiwa na serikali ya nchi hiyo la China National Biotec Group, zilitolewa kwa zaidi ya watu 35,000 huko Mashariki ya Kati.

Alisema chanjo yenye uwezo inayoendelezwa na Sinovac Biotech ipo katika awamu ya mwisho ya majaribio huko Marekani Kusini na Kusini Mashariki mwa Asia, na moja inayoendelezwa kwa pamoja kati ya CanSino Biologics na maabara ya Jeshi la Mapinduzi la Watu wa China, pia ipo katika awamu ya mwisho ya majaribio barani Asia na Ulaya.

Mtaalamu katika kongamano hilo alisema athari ijulikanayo kama ADE, athari inayopelekea shughuli za virusi kuimarika zaidi kutokana na matumizi ya chanjo, bado haijaripotiwa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uendelezaji wa Sayansi ya Tiba na Teknolojia, katika Tume ya Kitaifa ya Afya, Zheng Zhongwei, alisema China huenda itaweza kuzalisha dozi milioni 610 za chanjo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.