NEW DELHI,INDIA

CHINA  na India zimesema zimekubaliana kuupunguza mvutano uliozuka upya kati yao katika mpaka unaozozaniwa wa Himalaya na kuchukua hatua za kurejesha amani na utulivu kufuatia mazungumzo ya ngazi ya juu ya kidiplomasia yaliyofanyika Moscow.

Taarifa ya pamoja ya nchi hizo ilisema Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Wang Yi na mwenzake wa India S. Jaishankar walikutana mjini Moscow na kufikia muafaka wenye vipengele vitano, yakiwemo makubaliano kuwa wanajeshi kutoka pande zote waache mara moja kushambuliana na kutuliza mvutano.

Muafaka huo uliofikiwa pembezoni mwa mkutano wa Shirika la Ushirikiano wa Shanghai ulifanyika baada ya makabiliano kuzuka katika eneo la mpakani la magharibi mwa milima ya Himalaya mapema wiki hii.