NA MARYAM SALIM, PEMBA

CHOYO, roho mbaya na kutawaliwa na mfumo dume kwa wanawake ndio chanzo na sababu kubwa inayowafanya akinamama kukosa kuchaguliwa kwenye nafasi za uongozi katika majimbo husika”.

Hayo ni maneno kutoka kwa baadhi ya wanawake ambao tayari wameshawahi kugombea nafasi za uongozi katika majimbo mbali mbali.

Wlisema mambo hayo ndio chanzo kimoja kikubwa kinachowafanya wanawake kutowaunga mkono wanawake wenzao kushika nafasi za uongozi.

Bishara Muhamad Mussa mkaazi wa Tumbe, ni mwanamke jasiri mwenye kupenda wananchi wenzake hususan akinamama tayari ameshashika nafasi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kugombea jimbo la Tumbe kupitia chama cha Mapinduzi.

Alifahamisha kutokana na dhana potofu , roho mbaya zilizotawala miongoni mwa wanawake ndio chanzo kinachowakatisha tamaa kwa wale wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi.

“Miongoni mwetu sisi akinamama tumekuwa na roho mbaya na uchoyo pale tunapoona wenzetu wanataka kugombea Uongozi na hivyo tunawapa nafasi akinababa,” alieleza.

Akitolea mfano, Bishara alisema wanawake wengi hasa Kisiwani Pemba husema mwanamke sio kiongozi wala hafai kuongoza watu na badala yake nafasi hizo kuwaachia wanaume kila kipindi cha kugombea kinapofika.

“Mwanamke ni kiongozi na anafaa kuongoza kama wanavyoongoza watu wengine, hata hizo dini zinazotuongoza basi hazijamkataza mwanamke asigombee wala asichaguliwe, mwanamke anafaa na anastahiki kuchaguliwa kuongoza wenzake, ila tu asikiuke mipaka ya dini yake wala sheria za nchi na akaweza kuleta maendeleo,” alisema.

Kuhusiana nay eye mwenyewe alisema licha yakuwa alishagombea nafasi mbali mbali za uongozi kupitia Chama cha Mapinduzi lakini bado wanawake wenzake hawapo tayari kumchaguwa kwa kuwa wanaowachagua ni haohao jambo ambalo wanaochaguliwa wengi hukimbia majimboni.

“Mimi mwenyewe binafsi mwaka huu pia nimejaza fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi, katika Jimbo la Konde, lakini bado mfumo huo unaendelea kuwepo kwa wanawake wenzangu, bado hatujaelimika wala hatujui umuhimu wa kumchaguwa mwanamke katika nafasi za Uongozi,” alisema.

Nae Bikombo Hamad Rajab mwanamke aliyegombea nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Wawi Wilaya ya Chake Chake, alisema iwapo mwanamke amegombea nafasi ya uongozi kama hana pesa, basi inakuwa tatizo na hawezi kufikia lile lengo lake.

Alieleza kuwa licha ya wanawake kughilibiwa kwa pesa, nguo pamoja na vitu vyengine vya thamani, pia wanwake wenyewe wametawaliwa na choyo, ubinafsi ambao umejengeka ndani ya nyoyo zao na hivyo kutokuwa tayari kubadili mfumo.

 “Sisi wanawake wenyewe hatupendani tumekuwa na roho mbaya kupita kiasi, kwani kuna mitazamo mibaya hapo mbele baada ya kupata nafasi hiyo, mtu huona kwamba endapo atakupa kura utaondokana na umasikini kumbe sio kusudio kabisa,” alisema.

Alieleza kuwa licha ya akinamama kutandwa na roho mbaya, choyo, na ubinafisi , lakini hata kwa upande wao akina baba nao wanaonekana kuwa na roho mbaya kwa wanawake wanapowaona wanaingia kwenye nafasi za Uongozi.

“Tunawapatiliza na kuwasema wanawake wenzetu kwamba wamekuwa wa mwanzo kutowaunga mkono wanawawke wenzao katika kuwachaguwa kwenye nafasi za Uongozi, lakini hata wanaume wanawashawishi akinamama wasiwachaguwe akinamama wenzao bali wawachaguwe wao,” alieleza.

Aliwataka wanawake wasikubali kuburuzwa, siku ikifika wawachaguwe wanawake wenzao  ili wawaongoze majimboni waweze kusukuma  maendeleo kwa akinamama wenzao.

Alisema kuna ulazima gani wa kila kipindi wachaguliwe wanaume peke yao, na kujiona wao ndio wenye uwezo wa kuongoza watu majimboni, ni vyema kuwepo mabadiliko ya dhati katika Jimbo kwa wanawake kujikaza kuibadilisha dhana hiyo.

“Wanawake tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha tunawachaguwa wanawake wenzetu katika Uongozi, kwa maslahi ya kila mtu, pia wanaume nao wasiwe na ubaguzi wapatieni wenza wenu fursa hizo kwa mashirikiano kwani nao wanaweza kuongoza”, alieleza mgombea huyo.

Nae mwalimu wa madrasa Hamad Saleh Hamad mkaazi wa Kijiji cha Chwale Jimbo la Kojani, alisema sababu zipo nyingi zinazo wafanya wanawake kutowaunga mkono wanawake wenzao katika kuwachaguwa kwenye nafasi za uongozi ikiwa ni pamoja na roho mbaya na choyo.

Alieleza kuwa licha ya elimu inayotolewa na wanaharakati mbalimbali juu ya kuelimisha jamii kuhusiana na wanawake kupewa nafasi za uongozi lakini mifumo dume inatatiza hali hiyo.

Aidha alisisitiza akina mama kutoa ushirikiano kwa wanawake wenzao katika kuwaunga mkono kwenye Uchaguzi wa  Oktoba 28 mwaka huu, ili kupata mabadiliko ya kimaendeleo zaidi kwenye majimbo yao.

Nacho Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, kimewataka wanawake kuwaunga mkono wanawake wenzao waliogombea nafasi na vyama mbalimbali katika uchaguzi mkuu.

Asha Abdi ambae ni ofisa mwandamizi wa TAMWA, alisema wakati umefika sasa akinamama kuachana na mambo yasiyoleta maana kama kuwavunja moyo wanawake hasa wale wenye nia ya kugombea uongozi.

Alisema kwa sasa zana potofu hazina nafasi na kwamba huu bi wakati wa sayansi na teknolojia hivyo kuwapa nafasi wanawake ni mambo yanayotiliwa mkazo.