Wengi waachwa bila ya kazi, kipato

Baadhi watafuta kazi mbadala za kujipatia riziki

NA HUSNA MOHAMMED

“KWA kweli huu ugonjwa wa corona kwa kiasi kikubwa umenirudisha nyuma katika maendeleo yangu na sasa natafuta njia mbadala ya kuendesha maisha yangu”.

Hayo ni maneno ya Zainab Mtima ambae ni dereva wa taxi ambapo maisha yake anategemea kutokana na kazi hiyo.

Alisema ugonjwa huo wa corona umegharimu maisha yake hasa kutokana na kutowasili wageni kutoka nje ya nchi.

“Wateja wangu wengi ni wageni kutoka nje tangu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupungua ugonjwa huu sijapokea mgeni hata mmoja, jambo ambalo ni gumu kwangu katika kazi yangu hii”, alisema.

Zainab ambae ni mjane na mama watoto watatu alisema anafikiria kutafuta njia mbadala ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wateja wa ndani kupanda gari yake.

“Kwa kuwa gari yangu ni taxi najaribu kushawishi wateja hata wa ndani wapnde alimradi mkono uende kinywani”, alisema.

Nae Katibu Mkuu wa kundi la kutangaza utalii wa ndani kwa wageni linalojulikana kama (Zanzibar Mamas) Sharon Robert Mhina, alisema kundi hilo la wanawake watupu kwa sasa limepunguza kazi za kitalii baada ya corona kuathiri sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.

“Tulikuwa tukifanya kazi ya kutembeza watalii na wengi ni wanawake kutoka nchi mbalimbali lakini tangu kuja kwa corona hivi sasa tunafanya majani ya chai na kusambaza madukani”, alisema.

“Lengo letu ni kutangaza utalii wa ndani katika visiwa hivi tunawatembeza watalii maeneo ya vivutio na tayari tulikuwa tumekubalika mpaka nje ya nchi muda mfupi tulioanza, mana tulianza Disemba kwa hiyo mwezi Disemba mwaka huu tunatimiza mwaka mmoja”, alisema.

Alisema lengo la kundi hilo lenye wanachama 40 wanawake kwa sasa ni kuisaidia serikali kutangaza utalii wa ndani kwani kazi wanayoifanya ni kutembelea vivutio hivyo.

Nae Fatma Mwalimu ambae kazi yake ni kuuza batiki, kusuka nywele na kuwachora piko watalii katika eneo la Ngome kongwe ndani ya Mji mkongwe, alisema ingawa serikali imefungua utalii lakini bado utalii haujachanganya vyema.

“Tuna matumaini kuwa mwisho wa mwezi huu wa Septemba biashara inaweza kuchanganya lakini kwa sasa bado”, alisema.

Nae Dereva wa gari za kubeba watalii ya Private hire, Said Abbas, alisema amekuwa akipata oda ya wageni wachache jambo linaloonesha bado utalii haujachanganya licha ya wakati wa msimu wa utalii kwa sasa.

“Kipindi kama hiki unapata oda ya watalii muda wote, lakini kwa sasa kidogo tu unapata na siku nyengine hupati kabisa.

MARADHI YA CORONA NA UTALII WA ZANZIBAR

Baada ya kuanza kwa maradhi hayo mwezi Machi mwaka huu serikali iliweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuzuia uingiaji wa ndege ambazo mara nyingi zimekuwa zikileta watalii ikiwa ni pamoja na kupambana na ugonjwa huo usiendelee kuambukiza nchini.

Kama nilivyoeleza hapo awali, hivi sasa serikali imeanza tena kuruhusu uingiaji wa ndege za kitalii ambapo kwa kuanzia ndege za shirika la ndege la Ethiopian Airlines, shirika la ndege la Qatar air na mengineyo.

Maeneo mengi ya kitalii yanaonekana kurudi kama awali ingawa kwa taratibu sana kufuatia baadhi ya nchi za Ulaya kutoruhusu ndege zao kufanya safari za kitalii.

KUWASILI KWA NDEGE ZA KITALII ZANZIBAR

Kwa kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeruhusu ndege za kitalii na kibiashara kuingia nchini shirika la ndege la Gulstrem kutoka Austria imeanza safari zake katika uwanja wa Abeid Aman Karume.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea wageni kutoka Austria, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, Mulhat Yussuf Said, alisema, ndege hiyo ni ya kwanza kuingia nchini wageni walifuata masharti yote yaliyowekwa na serikali kabla ya kuingia nchini.

Alisema, katika ndege hiyo ilikuja na abiria kadhaa wakiwemo, watalii na waendesha ndege wawili ambapo wageni hao wataelekea katika hoteli za kitalii.

Aidha alisema kuja kwao wageni hao, kutaendeleza biashara ya utalii nchini ambapo takribani mienzi mitatu ilikuwa biashara hiyo imesitishwa kutokana na ugonjwa wa corona.

“Mwanzoni mwa Machi mwaka huu serikali ilipiga marufuku uingiaji wa ndege za kitalii na kibiashara baada ya kujitokeza mripuko wa janga la virusi vya corona ila imani yangu kwa sasa biashara ipo wazi na watalii wataendelea kuingia nchini” alisema.

Hivyo, aliwataka watalii kuingia nchini kupitia uwanja wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwani umezingatia usalama kwa watalii wanaoingia nchini.

Aidha alifamaisha kuwa wageni walioingia nchini awali walipimwa joto la mwili na kupakwa dawa wakati wakishuka katika ndege na baadae kuendelea na utaratibu uliokuwepo.

Sambamba na ndege hiyo, lakini shirika a ndege la Ethiopian airlines nalo pia linaleta huduma za usafiri Zanzibar na kwamba watalii na abiria kutoka nje wanawasili Zanzibar kipindi hiki cha kupungua ugonjwa wa corona.

Pia shirika la ndege la Qatar nalo limeanza kuleta watalii pamoja na wageni wakati huu wa kupungua kwa ugonjwa wa corona Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

WAFANYAKAZI WA MAHOTELI YA KITALII WANAZUNGUMZIAJE

Monica Kipambane anaefanya kazi katika hoteli moja ya kitalii Michamvi, yeye alisema kazi katika hoteli hiyo kwa sasa imefungwa na tangu kusitishwa kuja kwa ndege za kitalii bado hawajaanza kazi.

“Utalii uliporuhusiwa na ndege kuruhusiwa kuja Zanzibar tulifurahi sana, lakini mabosi wetu walitupigia simu tusubiri kwanza hadi mwezi wa Septemba”, alisema.

Nae meneja wa hoteli moja ya kitalii katika mji mkongwe wa Zanzibar ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema wamepata oda mwezi wa Septemba kupokea watalii wan chi mbalimbali ikiwemo Italia.

“Unajua baadhi ya nchi bado hawajafungua milango ya utalii hasa ndege zao kufanya safari nchi nyengine na ndio maana bado utalii wetu haujachanganya, lakini tuna Imani mwezi huu mwisho na mwezi ujao biashara itachanganya”, alisema.

KATIBU MTENDAJI KAMISHENI YA UTALII

Katibu Mtendaji kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk. Abdullah Mohammed alisema sekta ya utalii imepata athari katika kipindi cha maradhi ya corona hali ambayo ilipelekea uchumi wa nchi kupungua kwa asilimia tatu.

Alisema, hali imejitokeza kutokana na wananchi wengi wa Zanzibar kutoitilia mkazo dhana ya utalii kwa wote ambayo ndio dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kutegemea zaidi watalii kutoka nje.

Alisema pia corona imeonesha wazanzibari kuwa sio kitu ambacho wanachokiona ikiwemo wazungu wanaokaa mahoteli, wanaokuja kupitia viwanja wa ndege na bandarini pia hata gari zinazobeba abiria zinategemea sekta ya utalii.

Aidha, anabainisha kwamba, utalii ni sekta inayoengwa engwa na kuendelea kutegemewa lakini ni lazima wazanzibari wafahamu kwamba utalii wa ndani ni muhimu sana.

Hata hivyo, alisema baada ya kuwepo kwa maradhi hayo wananchi hasa waliokuwepo kwenye mnyororo wa uchumi ikiwemo wafanyabishara, wakulima, wachuuzi na watu wengine wamefahamu lengo la Rais kwa kufanya utalii wa ndani na kuwekeza wenyewe kwa kufanya utalii wa ndani kwa kutembea katika vivutio vyao.

“Kwa mfano China inategemea sana utalii wa ndani kuliko watalii wa kimataifa wanaokwenda nchini humo kutoka nchi mbalimbali na wanatosheleza kabisa kufanya soko la utalii na biashara zao zinakwenda,” alisema.

Alisema Zanzibar ni tajiri kwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii kwani mpaka sasa kisiwani Pemba ina zaidi ya vivutio 80 vya utalii na Unguja zaidi ya 100.

“Tungekuwa tunafanya utalii wa ndani na kujipanga kufanya utalii basi tungezuia wageni wasije nchini kwa sababu ya maradhi na ingekuwa corona haijaja kwetu basi wenyewe ingekuwa tunaendelea hapa hapa,” anasema.

Dk. Abdulla, aliwasisitiza wananchi wa Zanzibar wasitegemee wageni pekee na badala yake kubuni biashara nyengine na hata kuchora picha ambazo zinaendana na wazanzibari katika utalii wa ndani.

Hata hivyo, anaimani kuwa nchi za nje zitakapofungua milango yake ya utalii na kuruhusu ndege kuja hasa kwa kuwa balozi wa Italia ameona hali halisi ya utalii Zanzibar kwa ziara yake ya karibuni, ni wazi kuwa utalii utarudi tena kwa nguvu.

Nae Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali, alisema mara baada ya kuzuka ugonjwa wa corona hapa Zanzibar kumekuwa na changamoto kubwa hasa wanawake wengi kupoteza kazi zao za ujasiriamali.

“Wapo akinamama wengi wamejiajiri lakini corona imetibua shughuli zao hasa wa sekta ya utalii licha ya kufunguliwa shughuli za kitalii lakini huko duniani bado hali ni tete”, alisema.

“Kama tunavyojua corona bado ipo haijesha imepungua tu, milango ya utalii imeshafunguliwa, jamii itafute njia mbadala ya kuhakikisha wanafanya kazi zitakazowaletea tija”, aliongeza Dk. Mzuri.

HALI HALISI YA UTALII ZANZIBAR KABLA YA CORONA

Kabla ya ugonjwa huo kuingia duniani idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 376,242 mwaka 2016 hadi watalii 433,474 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 28.

Aidha Machi mwaka huu idadi ya watalii ingeongezeka na kufikia 800,000 lakini kutokana na janga hilo mwezi huo jumla ya watalii 20,584 ambapo mwezi Machi mwaka jana ni watalii 33,883 walioingia.

Hata hivyo, mwezi wa April mwaka huu, Zanzibar imepata athari ya kutoingia watalii na kutegemea utalii wa wageni kwani ilipokea wageni wasiozidi 300 wakati mwaka jana katika kipindi hicho walipokea wageni zaidi ya 2000.

Kuhusu idadi ya watalii kupanda kabla ya kuibuka kwa janga hilo, sera na mikakati ya serikali iliwataka watendaji waliyopewa majukumu ya kuutangaza utalii kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo.

Imefika wakati wananchi kujifunza kupitia janga hilo na kutilia manani maneno ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein kuwasisitiza wazanzibari kuthamini vitu vya kwao hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhamasisha utalii wa ndani.

Sekta ya utalii ni sekta inayochangia sana katika uchumi wa nchi hasa hapa Zanzibar ukiachilia zao la karafuu huku uchumi huo ukikuwa kwa wastani wa zaidi ya asilimia 7.

Utalii pia kwa Zanzibar unachangia pato la taifa kwa asilimia 27 na zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni zinapatikana kutokana na watalii wengi kupenda mandhari ya Zanzibar na utamaduni wake ambao una thamani huvutia takriban zaidi ya watalii 500,000 kwa mwaka.

Mapato hayo yanapatikana kwa watalii wenyewe kupitia viwanja vya ndege, bandarini, watembeza watalii sehemu mbalimbali ikiwemo katika mashamba ya viungo na maeneo mengine.

Hivyo, ni wazi kuwa baada ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa sasa kufungua milango wazi baada ya kupungua corona, tuna Imani kwamba utalii utarudi tena kama awali.