NA HABIBA ZARALI

MENEJA wa benki ya CRDB kanda ya mashariki,  Badru Iddi amesema, benki hiyo itaendelea kuboresha  huduma zake ili  kuwaondolea usumbufu wateja wake.
Alisema lengo la CRDB ni kuhakikisha huduma zao zinakuwa za kisasa kwa kuwawezesha wateja wao kupata huduma kwa haraka na kuongeza kipato katika nchi.


Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya QRCode uliofanyika katika ofisi za benki hiyo Chake Chake Pemba, ambapo huduma hiyo itamuwezesha mteja kutoa maoni katika mtandao  kupitia simu ya mkononi na kumrahisishia kupata huduma kwa haraka na kwa wakati.


Alifahamisha kuwa hapo awali wateja wao walikuwa wakitoa maoni kwa maandishi katika karatasi ambako imeonekana sio njia sahihi kwani huchelewesha kupata majibu kwa wateja hao.

“Sasa inamaana wateja wetu kupitia mfumo wa huduma hii ya QRCode  watatuma maoni yao kupitia simu ya mkononi na moja kwa moja yatafika katika ofisi zetu za makao makuu na mteja atajibiwa hapo hapo,” alisema.
Alielezea kuwa kuboreshwa huduma zao kumeanzia sehemu nyingi ikiwemo kuongeza wakala katika  wilaya zote za Pemba jambo ambalo linawarahisishia wateja kupata huduma kwa urahisi.
“Huduma hii mbali na kumrahisishia mteja kujibiwa haraka lakini pia inaongeza kipato katika nchi yetu,”alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa biashara kanda ya mashariki, George Yatera aliwataka wafanyabiashara kuitumia benki hiyo ili waweze kuongeza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

Alisema uchumi ni sehemu ya maisha na kukua kwake ndiko kunakoweza kuondoa umaskini kwa jamii na nchi nzima.
“Ni vyema wafanyabiashara ambao bado hamjaingia katika huduma za benki hii jaribuni muone ili muweze kunufaika na faida zilizomo,” alisema.

Mapema Meneja wa CRDB tawi la Pemba, Ahmada Ali Abubakar, alisema upendo kati ya wateja na benki hiyo ni sababu kubwa itakayoboresha huduma za benki hiyo.