NA MADINA ISSA

CHAMA cha CUF kimelaani kauli ya Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akisema kuwa inaweza kuhamasisha vurugu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumza na mwandishi wa habari, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Mussa Haji Kombo alisema kuwa Zanzibar inahitaji amani na utulivu hivyo kutokea mtu kutoa kauli ambazo sio njema haziwezi kuvumiliwa na chama chao.

“Chama cha CUF kimesikitishwa na kauli hizi ambazo kimsingi zinaashiria kuleta vurugu na taharuki ndani ya nchi yetu,” alisema.

Alifahamisha kwamba hoja ya pingamizi ni ya kisheria na imekuwepo tokea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi katika uchaguzi wa 1995, hivyo kutoa matamshi yenye azma ya kufanya vurugu kwa kisingizio cha kuwekewa pingamizi ni jambo lisilokubalika.

“Tukumbuke kwamba mwaka 2002, CUF iliwekewa pingamizi na Chama cha NCCR Mageuzi na kukosa wagombea wa majimbo matano, lakini hatukufanya maandamano ya kusababisha umwagaji wa damu, iweje kuwekewa pingamizi iwe ndio chanzo cha kuhamasisha vurugu na kusema liwalo na liwe?” alihoji Kombo.

Alifahamisha kuwa Zanzibar Januari 26 na 27 mwaka 2001, kulitokea vurugu zilizosababisha umwagaji wa damu ya wananchi katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema kuwa chanzo cha vurugu hizo ni kauli za uchochezi za kiongozi huyo na kupelekea maandamano ya umwagaji wa damu na kupelekea baadhi ya wananchi kukimbia nchi.

“Yaliyotokea wakati ule tusingependa yajirudie katika visiwa vyetu, kwani yalisababisha nchi yetu kwa mara ya kwanza kuzalisha wakimbizi na vizuka walio wengi,” alisema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Ali Makame aliwataka Wazanzibari wasikubali kauli za uchochezi ambazo zitaleta vurugu katika nchi yao ambayo imejengeka kwa misingi ya amani na utulivu.

“Viashiria vyovyote ambavyo vinaleta uvunjifu wa amani kwa mtu ambae mwenye kuitakia mema nchi yake hawezi kuvumilia na tunamuomba Msajili wa vyama vya siasa akiangalie chama hicho kwa umakini na lolote ambalo litatokea wao ndio wa kujibu”, alisema.