MNAMO mwezi Aprili mwaka 2020 wakati ugonjwa wa kuabukiza wa corona ulipoingia na kushika kasi barani Afrika, nchi Madagascar, ilitangaza kugundua dawa iliyotengenezwa kwa miti shamba ambayo inaweza kutibu ugonjwa huo.

Bila ya hofu na woga, rais wa nchi hiyo Andry Rajoelina akautangazia ulimwengu kwamba nchi yake imegundua dawa ya kutibu corona huku akiyaalika mataifa kwenda kununua dawa hiyo iliyotengenezwa kienyeji.

Baadhi ya nchi zikajitokeza kwenda kunua dawa hiyo kwa ajili ya kutibu raia wake walioambukizwa corona, lakini pia yapo mataifa barani Afrika yalinunua dawa hiyo kwa ajili ya utafiti.

Mashirika ya afya nchini Madagascar na hata yale ya kimataifa yalitilia shaka uwezo wa dawa hiyo ya kienyeji kutibu ugonjwa wa corona ambayo imetengenezwa kwa kutumia mti unaojulikana kama pakanga ama ‘artemisia’.

Taasisi ya tiba nchini Madagascar ‘Malagasy Institute of Applied Research’ (Imra), ilionyesha wasiwasi juu ya ufanisi wa dawa hiyo inayoelezewa na rais Andry Rajoelina kama yenye uwezo wa kuzuia na kupona corona.

Taasisi hiyo ilisema kuwa mitishamba inaweza kudhuru afya ya mtu kwani na kwamba hakuna ushahidi wa ufanisi wake kisayansi dhidi ya kutibu na kuponya corona.

Wakati akiipigia debe dawa hiyo, rais Rajoelina alisema, “Kinywaji cha dawa hii ya mitishamba huonesha matokeo katika kipindi siku saba”, huku akiwataka watu kuitumia kama hatua ya kujikinga na ugonjwa wa corona.

Akaongeza kueleza kuwa, “watoto wa skuli wanapaswa kupewa kinywaji … kidogo kidogo kwa siku nzima,” aliwaambia mabalozi na watu wengine waliokua wamekusanyika kwa ajili ya uzinduzi wa kinywaji hicho.

Kuali ya rais huyo ikapingwa na Prof. Brian Klaas, mtaalamu wa Madagascar katika Chuo cha London, ambaye alisema kuwa msimamo wa rais Rajoelina wa kuwataka watu watumie dawa hiyo unaweza kusawasababishia Wamadagascar madhara.

Mnamo mwezi Mei mwaka 2020, corona nchini Madagascar ikaripotiwa kuongezeka kasi ya maambukizi kufikia zaidi ya watu 15,000 na vifo kufikia zaidi ya watu 200, hiyo ikawa ni uthibitisho kuwa dawa iliyopigiwa debe na rais haifanyikazi ipasavyo.

Taarifa kutoka nchini Madagascar, zinaeleza kuwa hadi sasa bado hakuna ushahidi kwamba kemikali za mmea huo ambazo inaweza kudhibiti malaria pia zinaweza kutibu corona.

Mmea huu unatoka wapi? Mmea huo kwa jina kamili huitwa ‘artemisia annua na asili yake ni bara Asia, lakini hukuzwa katika maeneo mengi duniani yenye joto na jua.

Mmea huu umekuwa ukikuzwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika mashariki zikiwemo Kenya na Tanzania. Nchini China, mmea huo hufahamika kwa jina la  “qinghao.” 

Mmea huu umetumiwa kama tiba ya kiasili nchini China kwa zaidi ya miaka 2,000 kutibu magonjwa mengi, ukiwemo ugonjwa wa malaria, pia hutumiwa kupunguza maumivu na kudhibiti homa.

Kwa Kiingereza huitwa ‘sweet wormwood’ au ‘annual wormwood’, na baadhi ya watu wamekuwa wakiutumia kwa sababu mbalimbali kama tiba na hata kuongezwa kwenye vinywaji.

Kemikali iliyo ya nguvu hutolewa kwenye majani yaliyokaushwa ya artemisia annua na hufahamika kama artemisinin. Kemikali hiyo ndiyo inayotibu malaria.

Wanasayansi nchini Uchina waligundua nguvu za kemikali hiyo wakati wakitafuta tiba ya malaria miaka ya 1970.

Dawa zinazotumia Artemisinin kwa pamoja na kemikali nyingine, kwa kifupi ACTs, hupendekezwa na WHO kutumiwa dhidi ya malaria, ikiwa ni pamoja na aina ya viini vya malaria vilivyo sugu dhidi ya chloroquine.

Afrika, mataifa mengi huanza kwa kutumia Sulfadoxine pyrimethamine au Amodiaquine kutibu mgonjwa wa malaria kwanza na zikishindwa basi ACTs hutumiwa.

ACTs huwa na aina moja au nyingine ya artemisinin (aina kuu ni artesunate, artemether na dihydroartemisinin) na kemikali nyingine. Aina ya artemisinin hupunguza sana viini vya malaria katika siku tatu za kwanza na kisha kemikali hiyo nyingine huvimaliza viini vilivyosalia.

Upatikanaji wa ACTs kwa wingi katika mataifa yaliyoathiriwa sana na malaria umetajwa kama moja ya sababu kuu za kupungua pakubwa kwa watu wanaouawa na malaria duniani katika miaka 15 iliyopita.

Aidha, viungo halisi vilivyo kwenye dawa hiyo ya kinywaji kwa jina Covid-Organics havijulikani hasa, ingawa serikali ilisema asilimia 60 inatokana na mmea wa artemisia annua.

Madagascar pia imekuwa ikitengeneza tembe za Covid-Organics na hata dawa ya kudungwa kwa kutumia sindano. Rais Rajoelina anasema majaribio ya hiyo ya dawa ya kuchomwa mwilini kupitia sindano yanaendelea.

Wanasayansi kutoka Ujerumani na Denmark wamekuwa wakifanyia majaribio kemikali kutoka kwa mimea ya artemisia annua, na walisema mmea huo ulionyesha mafanikio dhidi ya virusi vya corona kwenye maabara.

Utafiti huo ambao haujahakikiwa na wanasayansi wengine ulibaini kwamba kemikali za mmea huo zilionyesha sifa za kukabiliana na virusi hivyo zilipotolewa kwa mmea huo kwa kutumia maji au kilevi.

Watafiti hao kwa sasa wanafanya kazi kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Kentucky kufanyia majaribio mmea huo kwenye binadamu.

Nchini Afrika Kusini, kuna wanasayansi wanaofanyia majaribio mmea wa artemisia annua na mmea mwingine unaokaribiana sana na huo – artemisia afra – kubaini iwapo unaweza kufanikiwa kutibu Covid-19. Utafiti huo unafanyika katika maabara lakini hakuna matokeo yoyote yaliyotolewa kufikia sasa.

WHO inasema hadi kufikia sasa hawajapokea taarifa zozote kuhusu majaribio yaliyofanywa na Madagascar kuhusu matumizi ya Covid-Organics dhidi ya virusi vya corona.

Jean-Baptiste Nikiema kutoka WHO kanda ya Afrika alisema kwamba shirika hilo huenda likahusika katika hatua za baadaye za majaribio ya dawa hiyo, lakini itategemea habari watakazozipokea kuhusu majaribio ya awali.

Lakini kwa sasa WHO wanasisitiza kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba dawa zinazotokana na artemisia hufanikiwa dhidi ya Covid-19.

Shirika hilo linaongeza kuwa tiba zote za miti shamba “zinafaa kuchunguzwa kubaini uwezo wake na madhara” kupitia majaribio yaliyofanywa kwa njia ya kisayansi.