NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imesema kuna jumla ya vituo tisa vinavyotoa dawa ya ‘methadone’ katika hospitali na nyumba 29 zinazotoa tiba ya uraibu wa dawa za kulevya nchini.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Wilbert Kaji wakati wa utoaji wa msaada kwa waathirika wa dawa hizo.

Alisema vituo tisa vinavyotoa tiba ya dawa hizo vipo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali ya Temeke, Mwanyamala, Mbeya, Mwanza, Tanga, Dodoma na Bagamoyo ambapo takribani waathirika 8,000 wanapatiwa huduma hizo kila siku.

Kamishna huyo alieleza kwa upande wa nyumba za utoaji tiba kwa watumiaji wa dawa hizo zipo 29, ambapo kati ya hizo nyumba tatu zinahudumia wanawake katika mikoa ya Kilimanjaro, Pwani na Dar es Salaam ambazo zina jumla ya wanawake 35.

Alisema katika kutekeleza suala la huduma za utengemano, Mamlaka kwa kushirikiana na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) pamoja na Flaviana Matata Foundation wametoa vifaa tiba vya kujikinga na magonjwa maambukizi ikiwemo corona pamoja na taulo za kike kwa waathirika wa dawa za kulevya.

Alifafanua kuwa, Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia mradi wa EU-ACT wametoa mashine 12 za kunawia mikono pamoja na sabuni zake kwa vituo vya ‘methadone’ ambapo mwanamitindo Flaviana Matata kupitia taasisi yake wametoa taulo za kike kwa wanaopata nafuu kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema tatizo la dawa za kulevya katika jamii ni suala la mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta mbali mbali katika kupambana nalo wakiwemo waathirika hao na jamii kwa ujumla.

Aliongeza kusema, serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli kwa kutambua athari ambazo husababishwa na tatizo hilo hasa kijamii, kiafya, kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia ilianzisha Mamlaka hiyo mwaka 2017.

Alitoa shukurani kwa wadau wote wa maendeleo ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Mamlaka katika jitihada mbali mbali za kupambana na tatizo la dawa hizo hususani Flaviana Matata ambae ameonesha uzalendo wa kipekee kwa kuwasaidia akinamama ambao wameathirika na matumizi hayo.