NA MARYAM HASSAN

VIJANA wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupatikana na vidonge 15,000 vinavyosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya.

Taarifa zilizotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Omar Khamis, alisema vijana hao wamekamatwa katika Bandari ya Malindi Unguja Septemba 14 mwaka huu majira ya saa 6:40 za mchana.

Akitaja majina ya vijana hao alisema Makame Ngwali Makame (24 mkaazi wa Bububu, Ali Hamad Salum (27) mkaazi wa Kwamtipura, Kheir Khamis Mwadini (30) mkaazi wa Mtoni na Abdillah Said Seif (19) mkaazi wa Fuoni.

Alisema wote kwa pamoja walikamatwa wakiwa wanasafirsha dawa za kulevya vidonge hivyo, aina ya Valium vinavyokadiriwa kuwa na uzito wa gramu 1.2.

Mkuu huyo alisema vijana hao walipatikana wakiwa wameficha ndani ya maboksi na kusafirisha kwa jahazi kutoka Bagamoyo kuja Zanzibar jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha, katika operesheni hiyo alisema Septemba 19 mwaka  majira ya saa 12:00 jioni huko Jang’ombe Mjini Unguja alikamatwa  Abdalla  Khamis  Said 22, mkaazi wa  Jang’ombe.

Alisema mtuhumiwa huyo amepatikana akiwa na mafurushi manne na vifuko vidogo vidogo vya plastiki yenye kuonesha ndani yake mkiwa na majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa 589gram.