NA LAILA KEIS

MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Hassan Ali Kombo, ameutaka uongozi na wananchi wa shehia ya Fukuchani, kuacha muhali badala yake kuwafichua watu wanaochimba mchanga pembezoni mwa fukwe za bahari.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, ofisini kwake Gamba, akieleza baadhi ya wananchi wa shehia hiyo kuchimba mchanga katika maeneo hayo na kupelekea uharibifu wa mazingira.

Alisema, kuna baadhi ya viongozi katika shehia hiyo, wana muhali na kufumbia macho vitendo hivyo ambapo kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria za nchi.

“Tunautaka uongozi wa shehia kushirikiana na wananchi, jukumu la kudhibiti kitendo hicho lianzie kwao wenyewe, waache muhali”, alisema.

Naye sheha wa shehia hiyo Haji Mohammed, alisema, tabia hiyo imeongezeka jambo ambalo linalopelekea uharibifu wa mazingira wa maeneo hayo.

“Mchanga wa fukwe hizo unapozidi kupungua itapelekea maji kujaa na kufikia majumbani, jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya wanakijiji hicho,” alisema sheha huyo.

Alisema wachimbaji wa mchanga huo, hufanya hivyo na kuuza kwa bei ya shilingi 1,000 kwa ndoo moja.

“Binafsi nishawakuta wanachimba na niliwapa onyo, pia niliwatishia kwa kuwapiga picha lakini waliacha siku moja tu na ya pili wakarejea tena, na mimi sitoweza kuwakamata kwa mikono yangu,” alisema.

Hivyo, alisema uongozi wa shehia hiyo, wapo katika mikakati ya kuweka ulinzi shirikishi ili kuwadhibiti wale wote wanaofanya kitendo hicho, na atakaekamatwa sheria itachukua mkondo wake.

Mmoja wa wakaazi wa kijiji hicho Fatuma Mngwali Khamis alisema watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wanatambulika, lakini watu wanaona muhali kuwataja hivyo aliwashauri wanakijiji wenziwe, kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo.