AMSTERDAM, Uholanzi
KOCHA wa zamani wa Ajax, Frank de Boer, ameteuliwa kuinoa timu ya taifa ya Uholanzi.
Bosi huyo mwenye umri wa miaka 50 amepewa mkataba wa miaka miwili ambao utamalizika mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022.
Kuteuliwa kwa beki huyo wa zamani wa Ajax na Barcelona kunachochewa na haja ya kujaza pengo la lililoachwa na Ronald Koeman aliyepewa mikoba ya Barcelona mnamo Agosti 2020 baada ya Quique Setien kutimuliwa Camp Nou.
De Boer aliwahi kucheza jumla ya mechi 112 akivalia jezi za Ajax, Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi. Aliwahi pia kuwafundisha Inter Milan ya Italia, Crystal Palace ya England na Atlanta United katika Ligi Kuu ya Marekani (MLS) kati ya Disemba 2018 na Julai 2020.
De Boer ndiye alikuwa kocha msaidizi wa Uholanzi wakati kikosi hicho kilipotinga fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini chini meneja, Bert van Marwijk.
Akipokuwa akiinoa Ajax kati ya Disemba 2020 na Mei 2016, De Boer alikiongoza kikosi hicho kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Uholanzi.
Mchezo wa kwanza kwa De Boer kuisimamia Uholanzi utakuwa wa kirafiki utakaowakutanisha na Mexico jijini Amsterdam mnamo Oktoba 7 kabla ya kuwaongoza vijana wake kuvaana na Bosnia-Herzegovina na Italia katika UEFA Nations League Oktoba 11 na Oktoba 14, 2020 mtawalia.(Goal).