CONAKRY,GUINEA

KIONGOZI mkongwe wa upinzani nchini Guinea Cellou Dalein Diallo anatarajiwa kuchuana na Rais wa nchi hiyo Alpha Conde katika uchaguzi wa Rais uliopangwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi ujao wa Oktoba.

Cellou Dalein Diallo alipitishwa katika chama chake cha Union of Democratic Forces of Guine (UFDG) kupeperusha bendera ya chama hicho na kuchuana na Rais Donde katika kinyang’anyiro cha urais.

Dalein Diallo (69) aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Rais Lansana Conte kuanzia mwaka 2004-2006 anatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa Conde hasa baada ya mpinzani mwengine aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi uliopita kutangaza kwamba, hatogombea uchaguzi wa mara hii.

Alpha Conde (82) ambaye alimshinda Diallo katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais 2010 na kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo mwaka 2015, hivi karibuni alikubali uteuzi wa chama chake wa kugombea muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi ujao.

Vyama vya upinzani nchini humo vinasisitiza kuwa, ni kinyume cha katiba kwa Conde kuwania muhula wa tatu kwa kuitumia vibaya katiba mpya ya nchi hiyo.

Mwezi Machi mwaka huu, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilitangaza kuwa asilimia 92 ya wapigakura waliunga mkono mabadiliko ya katiba katika kura ya maoni ambayo upinzani unasema kuwa ilimpa Rais Alpha Conde kibali cha kuendelea kutawala kwa miaka mengine 12.

Watu wasiopungua 30 waliuawa tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita katika maandamano ya upinzani ya kupinga mabadiliko hayo ya katiba.