NA KHAMISUU ABDALLAH
KATIBU Mkuu wa wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Zainab Chaula amesema hatua ya kuunganishwa kwa mkongo wa mawasiliano wa Taifa kwa Shirika la TTCL ni fursa kwa watoa huduma wa mitandao Zanzibar.
Kauli hiyo aliitoa katika utiaji saini wa makubaliano ya kuunganisha mkonga huo kwa TTCL Tanzania na Wakala wa Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), hafla ambayo ilifanyika katika ofisi za wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Kisauni, Zanzibar.
Alisema ni fursa ya kipekee kwa wawekezaji katika sekta mbalimbali Zanzibar na Tanzania bara kuitumia ili waweze kuwafikia watanzania na kulifikia soko kwa urahisi na haraka.
Dk. Zainab alibainisha kwamba pia uwepo wa mkonga wa Zanzibar ambao umeunganishwa kwenye mkonga wa mawasiliano wa taifa unatarajia kufungua fursa kwa wawekezaji na watoa huduma mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Aidha alisema mkonga huo wa mawasiliano wa taifa umetengenezwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 630 na wenye urefu wa umbali wa kilomita 7,910 na umefika kwenye mikoa 26 ya Tanzania bara.
Hata hivyo, alisema pia mkonga huo umefanikiwa kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati ikiwemo Rwanda, Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Malawi na Uganda.
Dk. Chaula alisema awali Zanzibar ilikuwa na changamoto ya mawasiliano iliyotokana na uwezo mdogo wa njia ya mawasiliano ya mawimbi ya radio (microwave redio) kutoweza kutosheleza mahitaji kwa sekta ya umma, binafsi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe, alisema, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetumia zaidi ya shilingi bilioni 30 kuunganisha mitambo hiyo katika mikoa yote ya visiwani vya Unguja na Pemba na wilaya zake.
Aliwataka wasimamizi wa mkonga huo kuhakikisha miundombinu hiyo wanaisimamia kikamilifu, weledi na ufanisi ili wananchi waendelee kunufaika na huduma za mawasiliano.