NA KHAMISUU ABDALLAH

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka msajili wa vyama vya siasa nchini kufanya utafiti ili kubaini vyama vya siasa Zanzibar na Tanzania vinavyotumia nafasi zao kwenye uwanja wa siasa kuhamasisha fujo na uvunjifu wa amani.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdullah Juma Saadala (Mabodi) aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Kisiwandui mjini Zanzibar.

Alisema msajili ndio msimamizi na mlezi wa vyama, hivyo ana wajibu wa kufanya utafiti ili kuvibaini vyama ambavyo vina nia ya kuleta fujo, vurugu, vituko na uvunjifu wa amani iliyopo nchini hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Namwambia msajili afanye utafiti wa kina na ikiwezekana achukue hatua inayostahiki kwa vyama vinavyotoa kauli na vitendo vya uvunjifu wa amani, fujo vituko na ubadhirifu wa mali za umma”, alisema.

Mabodi alisema CCM imegundua kuwepo viashiria vya kauli na vitendo ambavyo vinafanywa na baadhi ya wanasiasa na kushawishi wananchi kutaka kufanya fujo.

Aidha alisema CCM inasikitishwa na kauli za uchochezi zinazotolewa na watu ambao wamo katika vyama vya upinzani nchini kwa ajili ya kuchafua amani iliyodumu kwa muda mrefu.  

Alisema CCM ilikubali kwenda katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa ushindani kwa kushindana kwa sera na sio kauli ambazo hazina dhamira njema na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Tanzania tumekubali ushindani wa vyama vingi ili kuwe na vyama mbadala vya kutoa mawazo, lakini pia kuikosoa CCM ambayo ndio inayoongoza dola kwa sehemu ambazo zinastahiki kukosolewa, tunajenga nyumba moja ya utanzania na sote tunapita katika reli moja hivyo hatutamstahamilia mtu yoyote ambae ana nia ya kuiondoa amani ya nchi yetu,” alisema.  

Mbali na hayo Naibu Mabodi alibainisha kuwa CCM inaahidi kufanya kampeni na hamasa za kisayansi zitakazoendeleza amani na utulivu nchini kama ilivyokuwa kabla ya uchaguzi.

Hata hivyo, alisema ni imani ya chama chini ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa uchaguzi wa Oktoba mwaka huu utakuwa huru na haki.

Naibu Mabodi alisisitiza kuwa Chama cha Mapinduzi hakitakubaliana na mtu yoyote yule ambae atajaribu kuichafua amani ya nchi na kuahidi kutumia mbinu ambazo zitapelekea amani ya nchi kubaki salama.

Hata hivyo akizungumzia mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, alisema CCM itahakikisha mgombea wake Dk. Hussein Mwinyi anakubalika na ahadi anazozitoa kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema hayo yasingepatikana kama si kuthamini Mapinduzi, Muungano, utu na utaifa ambayo yamo katika kifungu kimoja cha amani, mshikamano, utulivu na ulinzi wa nchi hivyo CCM itasimamia hayo kabla na baada ya kampeni.

Mabodi alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa ukomavu wake na viongozi huku akivisihi vyama vyengine kutoibeza amani ya nchi ambayo ndio lulu kubwa kwa taifa la Tanzania.  

Alitumia muda huo kuwataka wagombea wa nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge kupitia chama hicho kuhakikisha wanapofanya kampeni kutoa ahadi kwa wananchi zinazotekelezeka ili waendelee kukiamini chama chao.