NA MWANDISHI WETU, MWANZA
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. John Pombe Magufuli, amesema hana wasiwasi wa kupata na ushindi wa chama chake kutokana na mambo mengi ya maendeleo yaliyoyafanywa ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Dk. Magufuli ameeleza hayo jana katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, wakati akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka huu.
Alisema wakati akiiingia madarakani miaka mitano iliyopita, Tanzania ilikuwa katika kundi la nchi masikini, lakini hivi sasa imebadilika kuwa na uchumi wa kati, kutokana na kuanza kukuwa.
Alisema alipoingia madarakani aliahidi kuifanya Mwanza kuwa kitovu kikuu cha biashara jambo ambalo amefanikiwa kwa kuimarisha miundo mbinu ya maji, elimu, na barabara, inayoruhusu malori yanayoenda nje ya nchi ikiwemo Kenya.
Alisema upande wa usafiri wa majini serikali katika Mkoa huo, imejenga chelezo pamoja na kununua meli tano moja ikiwa ni kubwa yenye thamani ya shilingi bilioni 1.53 sambamab na kuimarisha usafiri wa reli.
Alisema daraja la Kigogo limeanza kujengwa ambapo litagharimu shilingi bilioni 300 na likikamilika litapunguza kuvuka kwa meli na badala yake watu watasafiri barabarani.
“Serikali pia imetenga shilingi bilioni 15 kuweka meli kubwa ya Mv. Umoja ambayo itakuwa ni ya kubeba mizigo na kuwa mabehewa ya ili iweze kuondoka kwa haraka na gharama ndogo kwani tani moja hivi sasa inabebwa kwa shilingi 130,000 lakini itapoanza kazi tani moja itabebwa kwa shilingi 27,000.
Akizungumzia maendeleo ya sekta ya anga, Dk. Magufuli alisema upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza wenye urefu wa kilomita 2.8 umeanza na utakuwa na kilomita 3.5.
Alieleza kuwa upanuzi huo unakwenda sambamba na uwekaji rada, miundombinu ya kuhifadhi minofu ambapo ndege kubwa zinatua Mwanza na zitasafirisha tani 109,000.
Kwa upande wa huduma za jamii, Dk. Magufuli alisema serikali imeimarisha majengo mbalimbali ikiwemo la Oxygen, huku Seketure ujenzi wake unaendelea ikiwemo jengo la kina mama na watoto, wataalamu wa afya 147 wameongezwa na magari ya kubebea wagonjwa ambayo yapo kila Wilaya.