NA KHAMISUU ABDALLAH
WAKATI kampeni za uchaguzi mkuu wa Zanzibar zikianza rasmi leo, mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi, amewataka wanachama wa chama hicho waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kupiga kura ili kukipa ushindi wa kishindo chama hicho.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Kwahani katika ofisi za CCM mkoa wa mjini Amani na kueleza kuwa hakuna sababu ya mwanaCCM aliyefikia hatua hiyo kutopiga kura kwa kubaki nyumbani siku hiyo.
Mgombea huyo ambae kabla ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chana hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu alikuwa mbunge wa jimbo hilo hivyo kutumia fursa hiyo kuomba wananchi na wanachama wa jimbo hilo kuendelea kushirikiana nae kwa kujitokeza kumpa kura.
“Twendeni tukafanye uchaguzi huru na tuondoe malalamiko kwa kupata ushindi wa kishindo ambao haujawahi kutokea,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema jimbo la Kwahani ndio jimbo namba moja kwa mkoa wa Mjini kukipatia chama kura nyingi katika kila chaguzi zilizopita, hivyo aliwaomba kutomuangusha.
“Safari hii hakuna kulala kwa sababu mgombea urais wa Zanzibar anatokea jimbo lenu hivyo mnatakiwa kufanya kazi ya ziada kwa mabalozi, kamati za siasa, kamati za matawi na watu wote kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa ushindi wa kishindo unapatikana,” alisema.
Hata hivyo, aliwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumuamini na kumchagua kuwaongoza kwa kipindi cha miaka 15 na kuahidi kuendelea kuwatumikia bila ya kujali tofauti zao.
“Niwashukuru sana kwa mapenzi mlionionyesha kwa muda wote ambao nilikuwa nikiwatumikia na niwashukuru kwa dua zenu mpaka sasa nimeweza kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM naamini mtaendelea kuniunga mkono nami sitawaangusha,” alisema.