NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amesema endapo wananchi wa Zanzibar watamchagua basi atahakikisha kila manispaa na halmashauri zinajengwa masoko ya kisasa kwa wafanyabiashara wadogo.

Alisema, mpango huo unaendana na utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020 inayotilia mkazo juu ya kuimarisha uchumi wa wafanyabiashara wadogo na fursa muhimu ya kuongeza pato la serikali.

DK. Mwinyi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Kijangwani na Saateni ikiwa ni muendelezo wa ziara za kampeni za kisayansi za kuwafata wananchi wa chini kusikiliza kero zao.

Alisema serikali ya awamu ya nane itahakikisha kuwa masoko hayo yanakuwa na mazingira mazuri kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao na kuwa na huduma zote muhimu ikiwemo vyoo na miundombinu mingine.

Alisema anaamini kwamba wajasiriamali wadogo ni wengi Zanzibar ikilinganishwa na wajasiriamali wakubwa, hivyo ni lazima kuweka mkazo kwao ikiwemo kuwawezesha kiuchumi ili wafanye biashara zao bila bughudha.

“Nitahakikisha kuwa masoko hayo yasiwe ili mradi soko tu bali liwe soko ambalo lipo kwenye sehemu ambayo kuna biashara ya kutosha na karibu ya vituo vya daladala,” alisema.

Alisema, soko hilo la Kijangwani ni soko ambalo limewekwa kwa kipindi cha maradhi ya corona ili kuepusha msongamano wa watu kwenye masoko makubwa, hivyo aliahidi kuwa watapatiwa sehemu nyengine ambayo itakuwa ni sehemu ya kudumu.

“Ondoeni hofu, hali hii ilikuwa ya muda kwa sababu ya maradhi ya corona na sasa hivi maradhi hayo yamepungua, kwa kipindi hiki tunakabiliwa na uchaguzi, hivyo nikichaguliwa na kuwa rais wa Zanzibar mtapata habari zangu,” alisema.

Akizungumzia changamoto ya kutozwa shilingi 1,000 kila siku, Dk. Mwinyi alisema tayari serikali ya awamu ya saba imeshatengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara hao kupatiwa vitambulisho maalum ambavyo watalipia mwaka mzima kwa shilingi 30,000.

Alisema ili hayo yaweze kutimia ni vyema kwa wafanyabiashara hao kukichagua Chama cha Mapinduzi kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani ili waweze kushirikiana katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi.