Aahidi kubadilisha maisha ya vijana

NA ASIA MWALIM

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amesema endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, ataufanyia mageuzi mfumo wa elimu ili uweze kutoa manufaa zaidi kwa vijana.

Dk. Mwinyi alieleza hayo wakati alipopiga simu kuchangia kwenye kongamano lililowashirikisha vijana lililofanyika katika ukumbi wa Idrissa Abdul-wakil uliopo Kikwajuni mjini Zanzibar.

Mgombea huyo alipiga simu ya moja kwa moja wakati kongamano lililowashirikisha vijana lilipokuwa likiendelea ukumbini hapo, ambapo alisema ana dhamira ya kuufanyia mageuzi mfumo wa elimu akiamini kwamba ndio msingi wa kuwaletea maendeleo vijana.

“Vijana wawe na matumani na matarajio makubwa, nawaahidi endapo nitashinda nafasi ninayowania tutahakikisha wanapata elimu itayogeuza maisha yao”, alisema Dk. Mwinyi.

Alisema umefika wakati kwa vijana wanapomaliza elimu ya juu wawe na ujuzi na maarifa ambayo yatawawezesha kujiajiri wenyewe hali itakayowawezesha kujitegemea maisha yao.

“Naelewa changamoto ya ajira inayowakabili vijana, ili waweze kuajiri na kuajiriwa, lazima wawe na elimu na fani mbalimbali kama vile ufundi, utalii, uvuvi na utaalamu wa gesi na mafuta”, alisema.

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amewahimiza vijana kuhakikisha wanafanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura kwa kuchagua viongozi watakaosaidia kuleta maendeleo.

Alisema umefika wakati kwa vijana kuchagua viongozi wenye sifa nzuri zikiwemo kudumisha amani, utulivu, mshikamano na maendeleo ya nchi tuliyo nayo sasa na sio kushawishika na siasa za chuki kwa wasiopenda maendeleo ya nchi.

Alifahamisha katika muelekeo wa kupata viongozi bora kunahitajika siasa safi ambayo imo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sera yake inayokubalika, ilani inayotekeleza na hatimae kupata viongozi watekelaziji wa sera na ilani hiyo.