NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Mwinyi, amewaomba wana-CCM na wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu, ili kutimiza matakwa ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana mara baada ya kurejesha fomu za kuomba uteuzi kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambapo alisema siku hiyo ikifika wana-CCM na wananchi wakapige kura kwa Chama cha Mapinduzi.

Alitumia fursa hiyo kueleza kuwa endapo wananchi wa Zanzibar watamchagua na kumpa fursa ya kuwa rais wa Zanzibar, atakuwa tayari kuwasikiliza changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi kadiri itakavyowezekana.

Alisema ameomba nafasi hiyo akiamini uwezo wa kuwaongoza Wazanzibar anao, nguvu za kuongoza anazo na uwezo wa kutatuta changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi anazo.

“Nawaomba wana-CCM na wananchi wote, Oktoba 28 ikifika wakachague viongozi wa CCM, kwani ndio wenye uwezo wa kuivusha Zanzibar salama”, alisema.

Katika hatua nyengine, mgombea huyo aliwapongeza wana-CCM na wananchi waliomdhamini ili kukamilisha sharti la kisheria la fomu ya kuomba uteuzi wa nafasi hiyo na pia kuwapongeza wale waliokuwa na nia ya kumdhamini lakini hawakupata fursa hiyo.

“Walionidhamini wametosha, nathamini dhamira yenu njema kwangu hivyo sasa kazi iliyobaki ni kuhakikisha Oktoba 28 mnajitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura ili tuweze kuunda serikali na kuwatumikia wananchi,” alisema.

Mbali na hayo alisema katika uchaguzi wa mwaka huu CCM itafanya kampeni za kistaarabu zilizojaa amani na utulivu na kusisitiza kuwa haitafanya kampeni za matusi na kupakana matope.

Hivyo alivisihi vyama vyote vya siasa kuhakikisha wanafanya kampeni kwa amani ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki salama wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

“Mimi nivisihi vyama vyote vya siasa na wananchi wahakikishe kuwa tunafanya kampeni kwa amani na CCM, ina kampeni ya kisayansi na kwamba wataiona wenyewe nisiseme sana,”alisema

Awali Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, alisema ZEC baada ya kujiridhisha na ujazaji wa fomu za uteuzi, Septemba 10 itaweka wazi kwa muda wa masaa 24 fomu za mgombea huyo ili kutoa nafasi kwa wagombea wengine kuweka pingamizi.

Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018, kifungu cha 50 kinachoeleza huku uteuzi wa wagombea utafanyika Septemba 11 mwaka huu kama inavyoelekeza katika ratiba ya uchaguzi.  

Aliimtaka mgombea huyo kupeleka mwakilishi wake katika mkutano wa kupanga ratiba ya pamoja na kitaifa ya mikutano ya kampeni za uchaguzi zitakazoanza Septemba 11 mwaka huu hadi Oktoba 26.

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa mkutano huo utafanyika katika taasisi ya maendeleo ya utalii Maruhubi ambayo ndio itakuwa kituo cha waandishi wangaalizi na matokeo ya uchaguzi kwa mwaka huu.

Mgombea huyo alijaza fomu na kuweka saini tamko la kutokujihusisha na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi wakati wa uchaguzi na kujaza fomu ya tamko la kuheshimu utekelezaji wa maadili ya uchaguzi ambayo yamewekwa saini na pande zote ikiwemo vyama vya siasa, serikali na ZEC.