NA MWANTANGA AME, PEMBA
MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kwa Chama cha CCM, Dk. Hussein Mwinyi, amesema amepata matumaini makubwa ya ushindi wa kishindo kwa CCM utaotokana na wananchi wa Kisiwani Pemba kuonyesha kumuunga mkono katika uchaguzi Mkuu ujao.
Dk. Hussein aliyasema hayo katika Kongamano la Wanawake kisiwani humo lililotayarishwa na Jumuiya ya Wanawake, lililofanyika huko katika ukumbi wa Makonyo Chake chake Kisiwani Pemba.
Dk. Mwinyi alisema amekubaliana na tathmini ya awali aliyoifanya kisiwani humo, kwa wananchi hasa wanawake kuonyesha kumkubali kuwa Rais wa Zanzibar.
Alisema Pemba imeonesha kuwa na mabadiliko yatayokifanya Chama cha Mapinduzi kupata kura nyingi kisiwani humo kwa vile wananchi wameanza kutambua ukweli wa wanasiasa waliokuwa wakiwaunga mkono kukosa muelekeo wa kuwatumikia vyema wananchi.
Alisema akiingia madarakani atahakikisha kisiwa cha Pemba kinapata mabadiliko ya maendeleo kwa vile tayari ilani ya uchaguzi atayoitekeleza ina mambo mengi yanayohitaji kufanyika yatayowapa neema kubwa wanawake wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Akiendelea Dk. Mwinyi alisema katika kufanikisha adhma hiyo, anakusudia kuwapa nafasi mbali mbali za uteuzi, akiingia marakani na hana wasi wasi na hilo kwa vile wanawake wa kisiwa hicho wanamkubali.
Alisema wanawake wanakila sababu ya kufurahia ahadi hiyo, kwa vile ana dhamira ya kweli ya kuwainua wanawake katika serikali yake kwa vile ni wenye kujiamini, wakweli na waaminifu katika kutekeleza majukumu yao ya kikazi.