NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amesema serikali itaweka mfumo wa kuwatambua vijana wanaofanya biashara ya bodaboda kutambulika kisheria.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Paje ikiwa ni miongoni mwa kampeni za uchaguzi mkuu alipofanya ziara ya kusikiliza kero za wananchi katika mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema, waendesha bodaboda ni moja ya ajira ambayo inamuwezesha mwananchi kupata kipato cha kujiendesha katika maisha yake hivyo hakuna sababu ya kutotambulika na kutokuwa katika mfumo rasmi.

Aidha alisema ni lazima wafanyabiashara hao wawe na usajili na kutambulika kisheria kwani wanafanya kazi ya halali ya kujipatia kipato na kwamba bodaboda ni biashara kama nyengine ambayo inawasaidia wananchi kwa maeneo ambayo hayafiki usafiri wa gari za abiria.

Alisema serikali ya awamu ya nane atakayoiongoza baada ya ushindi wa uchaguzi mkuu itaimarisha maisha ya wafanyabiashara wadogo wakiwemo wajasiriamali ili waweze kunyanyuka kimaisha na kujiendeleza kiuchumi.

Akizungumzia ufinyu wa wafanyakazi wa afya, nyumba za wafanyakazi na jengo la kusubiria wagonjwa katika kituo cha afya Paje, Dk. Mwinyi aliahidi kuimarisha huduma hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Alieleza kuwa kufanya hivyo kutakwenda sambamba na kuimarisha majengo na vifaa tiba ili vituo vyote vinavyotoa huduma bora na kupunguza masafa kwa wananchi.

Kwa upande wa zao la mwani Dk. Mwinyi, aliwahakikishia wakulima wa zao hilo kuwajengea kiwanda cha mwani kama kilichokuwepo kisiwani Pemba, kupata bei nzuri ya zao hilo na masoko ili waweze kujiendeleza kimaisha na kujipatia maendeleo.

“Sio kiwanda tu bali tutawawezesha wakulima wetu kupata taaluma ya ukulima bora wa zao hili kwani eneo hili kwa kiasi kikubwa linawasaidia kinamama kuweza kujiajiri na kujipatia kipato sasa wanahitaji msaada na haki ya kutumia fukwe,” alisema.

Hata hivyo Dk. Mwinyi aliipongeza serikali ya awamu ya saba kwa kazi nzuri iliyofanywa katika utekelezaji wa ilani ya kupeleka huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo umeme na maji na kuahidi serikali ya nane itamalizia pale palipobakia.