NA HABIBA ZARALI, PEMBA
WANANCHI Kisiwani Pemba wamesema wamejenga imani kubwa na Mgombea Urais wa Zanzibar, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Husein Ali Mwinyi, kutokana na ahadi zake zenye kuleta maslahi mazuri ya wazanzibari.
Walisema nyota njema huonekana asubuhi, jambo ambalo ndilo lililoonekana kwa mgombea huyo tokea kupitishwa kwake mjini Dodoma hadi hivi sasa ni kwamba anakubalika kwa njia zote.
Kauli hiyo zilielezwa na baadhi ya wananchi waliohudhuria katika mkutano wa kampeni wa chama cha CCM iliofanyika Gombani ya kale Chake chake Kisiwani Pemba, ikiwa ni mara ya kwanza kuziduliwa kwa chama hicho kisiwani humo.
Abrahman Makame kutoka Kiwani alisema ahadi za Dk, Mwinyi ni za kuleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Zanzibar, jambo ambalo linawapa moyo mkubwa wa kumchaguwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Alifahamisha kuwa kauli yake ya kusimamia wabadhirifu wa mali na wala rushwa endapo ataitekeleza kwa vitendo maendeleo na yatazidi kuliko sasa.
“Tunachotegemea kwake Dk, Mwinyi ni mashirikiano zaidi hasa kwa kauli zake katika kampeni” alisema.
Rahma Hafidh Mohamed ,mkaazi wa Msuka Wilaya ya Micheweni, alisema tatizo la wananchi wa Kisiwa cha Pemba ni kupata maendeleo ambayo yatawawezesha kuendesha maisha yao vizuri, jambo ambalo kwa Dk, Mwinyi ndio tegemeo.
Akitowa wasiwasi kuhusu kumchaguwa mgombea huyo alisema kuwa asiwe na hofu, kwani hawawezi kufanya kosa kwa kumchaguwa asiyekuwa yeye.
“Wala asiwe na wasiwasi Dk, Mwinyi tutahakikisha tunae bega kwa bega mpaka tumpeleke Ikulu,”alisema.
Akizungumzia furaha yake mkutano hapo Mwenyekiti wa jumuiya ya wasioona, alisema amepokea ujumbe wa kuitwa na mgombea huyo yeye na wanachama wake ni jambo la faraja ambalo hajawahi kuipata.
Alisema si kitu cha kawaida kuona mgombea Urais kuwaita na kuwashirikisha katika masuala mbalimbal,i jambo ambalo kwao ni faraja kubwa.
“Nimepata ujumbe sasa hivi apa mkutanoni nilipo, kuwa kesho mgombea anataka kukutana na jumuiya hii sasa hilo sio jambo la kawaida kwetu tunaamini kuwa neema inakuja”alisema.
Amina Bakar Juma, mkaazi wa Wete alisema anaamini Dk, Mwinyi ataendeleza mazuri yatakayoachwa na Dk, Shein, ili kufikia katika hali nzuri kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Salim Fakih mkaazi wa Konde alisema juhudi na maarifa yanayofanywa na Rais wa awamu ya Saba ataweza kuyarithi Mwinyi hivyo wanaimani nae sana .
Wakizungumzia suala la amani na utulivu kwa nchi, Amina Haji Kheir mkaazi wa Mkoani alisema ni vyema kuendelezwa na wananchi wote kwani kuondoka kwake ni vigumu kurejea.
Alisema ni jambo la busara wananchi kufanya kampeni za kistaarabu kila mmoja kunadi sera zake, ili wananchi kuweza kumchaguwa wanaempenda.
“Tunajuwa kama Chama chetu cha CCM kina sera na ilani nzuri ambazo zinatekelezwa sioni sababu kishindwe”,alisema.
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wananchi mbalimbali wa mikoa miwili ya kisiwa cha Pemba ulikuwa ni wa aina ya kipekee ambao uliweza kuwaonesha njia sahihi ya kuweza kuchaguwa kiongozi sahihi atakae waongoza Wazanzibar miaka mitano ojayo.