NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar serikali yake itaondoa dhulma na upendeleo hasa katika upatikanaji wa ajira serikalini.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kusini kwenye ziara aliyoifanya ya kusikiliza kero za wananchi katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.

Alisema serikali atakayoiongoza atahakikisha suala la upendeleo wa ajira linaondoka na kwamba kila mwenye haki na sifa ya kuajiriwa atapata nafasi hiyo kwa misingi ya sheria na sio kwa upendeleo

Alisisitiza kuwa amegombea nafasi hiyo kwa dhamira ya kuwatumikia wazanzibari na sio vyenginevyo ikiwemo kusikiliza changamoto za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Aliwaeleza wananchi wa wilaya hiyo kwamba wanapaswa kumuamini na namna bora ya kuonesha imani ni kwenda kukipigia kura Chama cha Mapinduzi Oktoba 28 mwaka huu ili akatimize malengo hayo na mengine yenye maslahi ya wananchi wote.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi hao kwamba kiongozi yoyote atakayemteua kwa kumpa nafasi ya kuongoza na kusimamia majukumu, anapaswa kutekeleza wajibu huo na akishindwa kutatua changamoto za wananchi hatokuwa na nafasi.

“Haiwezekani uwe na wawakilishi katika wilaya na mikoa halafu unalazimika kuwa pale, wao wana kazi gani hili sitalivumilia. Lengo langu ni kuona kila mtu anawajibika katika sehemu yake na kama hatowajibika atachukukuliwa hatua”, alisema.

Akizungumzia suala la uwekezaji katika ukanda wa utalii, Dk. Mwinyi alisema serikali atakayoiongoza itaweka mfumo maalum ikiwemo wawekezaji kupewa kibali maalum ili utalii wanaouleta uwananufaishe wazanzibari kiajira na kibiashara.

Dk. Mwinyi akizungumzia maeneo yanayouzwa kwa ajili ya uwekezaji alisema serikali ya awamu ya nane itaweka mfumo kwa wawekezaji hao ili waliyopewa wanayatumia kwa shughuli za utalii na sio vyenginevyo.

“Wawekezaji tunawataka na kuwahitaji, hatutaki watu wachukue ardhi bila ya kuiendeleza hatutaki wawanyime fursa za ajira wazawa, tukibaini wanafanya hivyo hatutawavumilia”, alisema.